Kitu kimoja kiko wazi.
Chadema kama taasisi imechukua uamuzi sahihi. Kaulimbiu ya CCM ya tangu Aprili
2012 ni eti "Umoja ni Ushindi" hivyo malumbano ya kutuhumiana ufisadi
na ugamba yanabomoa umoja na kupunguza uwezekano wa ushindi kwa hiyo lazima
kuwavumilia viongozi wandamizi walio na nguvu ndani ya CCM vile kuwavua vyeo
vyao katika chama kutatufanya tushindwe kushinda katika chaguzi.
Chadema imetekeleza
kaulimbiu mbadala na kusema; hapana, viongozi wandamizi wanaocheza karata nje
ya uwanja na kuandamwa na tuhuma za usaliti tutathubutu kuwavua uongozi hata
kama hilo litayumbisha chama kwa muda kwa sababu ya umaarufu wao au kuwa kwao
na uwezo mkubwa wa uchambuzi wa mambo hautakizua chama kama taasisi kuwavua
vyeo au hata kuwafukuza uanachama.
Mfano wa Dakta Salim Ahmed
Salim ni muafaka hapa. Alipigwa vita na kutuhumiwa hata mauaji ya mwaasisi wa
Zanzibar ya baada ya Mapinduzi lakini hata baada ya kuzushiwa mambo mengi ya
hovyo na mwisho wa siku CCM kikashinda uchaguzi 2005 bendera yake ikipeperushwa
na mgombea ambaye hakuwa na sifa za uadilifu na umahiri wa uchambuzi wa masuala
ya kitaifa na kimataifa wa kulingana na wa Dakta Salim Ahmed Salim . Lakini
vile yeye ni mwenye hulka ya unyenyekevu na kutojiona bora kuliko wenzake na
kutotawaliwa na dhana ya kuwa bila yeye kuwa Rais basi hakuna la maana chama
chake kingeweza kikafanya, aliendelea kuwa mwanachama wa CCM na mwaka 2010
alijitokeza kumpigia kampeni ya urais kipindi cha pili mgombea ambaye mtandao
ulimbeba 2005.
Bila shaka mgombea wa urais
wa CCM wa 2005 na 2010 alinufaika na kuchafuliwa kisiasa kwa Dakta Salim. Labda
tofauti ya wale waliovuliwa uongozi na Chadema na Dakta Salim Ahmed Salim ni
wao kutokuwa na nidhamu ya kichama cha ukombozi ambayo inadai kuwa au ujiondoe
kama hujaridhika na uongozi uliopo au ukibaki basi uwe tayari kuvumilia kuchafuliwa
na wale wasio na uwezo wa kiakili kama wewe pale unapotaka kuwaondoa madarakani
tena kwa kucheza nje ya uwanja wa mchezo wa siasa unaofuata sheria zinazotungwa
na wale wale ambao kwa wakati huo ndio wenye uwingi wa kura katika vikao halali
za chama husika.
Vinginevyo wewe utakuwa
unakisaidia chama tawala cha CCM kwa kuanzisha zogo kuhusu eti mapungufu ya
viongozi waliopo kwa kujiaminisha kuwa wewe ni bora kuliko wao ambapo na wao
wanajiona ni bora kuliko wewe. Kwani Kambona si alikuwa kiongozi mahiri na
mwenye maono kuliko hata wazee wetu kama Mzee Kawawa? Lakini historia ya TANU
ikiandikwa yeye ataonekana msaliti na Mzee Kawawa ataonekana shujaa, siyo?
Kwani Rais Reagan na Rais George Bush ndio walikuwa wenye akili na umahiri
kuliko viongozi wa Republican Party ya enzi zao au ndio walikuwa muafaka
kuongoza ili kuleta umoja ndani ya chama?
Alipokufa Dakta Mondlane ni
kwa nini wasomi kama Marcelino dos Santos walimpisha Samora Machel kuongoza
Frelimo kama si kutii dhana ya nidhamu ya juu ndani ya chama cha ukombozi
kuzuia kuanzisha migogoro inayowasaidia watawala wa wakati huo kujinadi kama
wenye utulivu na hivyo kutokuwepo na mbadala. Kwa nini hadi leo Malkia wa
Uingereza ni mama Elizabeth badala ya Prince Charles? hivi kuongoza taasisi
lazima aliyeonekana anafaa lazima awe mwenye akili au umahiri wa uchambuzi wa
mambo kuliko wenzake?
Kuanzisha mtandao wa siri
wenye lengo la kubadili uongozi wa juu wa chama cha ukombozi ni usaliti na
anayeandaa mkakati huo wa siri hawezi kujinadi kama eti mwanademokrasia, yeye
ni mwanamakundi ya siri siri ndani ya chama husika kama hao anaowatuhumu yeye
kuwa na makundi yao yakuwadumisha kwenye uongozi. Haiwezekani kusema ni sawa
kutumia mbinu za kisirisiri nje ya utaratibu uliopo halafu ukajinadi kuwa
mtetezi wa demokrasia na wenzako eti wahafidhina.
Ningewaelewa hawa
waliovuliwa uongozi kama wangejenga hoja hiyo ndani ya chama chao kwa uwazi
kabisa na hoja hiyo ikikosa kupata kuungwa mkono basi wangetulia na kujaribu
tena na tena hadi hoja yao ipate kuungwa mkono na wajumbe wengi wa vikao husika
vya chama chao. Vinginevyo wangejitoa uanachama wa chama husika. Hivyo ndivyo
mwanademokrasia anavyotarajiwa kufanya. Mimi nilijitoa TANU tangu 1973 na
sijarudi CCM hadi leo vile najua hoja zangu zitakuwa na uungwaji mkono finyu
kwa sasa katika vyombo vya maamuzi, labda pale CCM kikiondolewa madarakani
kikabaki na waumini wa kweli wa ujamaa na umajumui wa kiafrika.
Kama wewe ni akina Abdul
Nasser anayepanga mapinduzi ya kutumia nguvu kisisiri basi sema hivyo nayo
inaitaji ujipange kufanikisha hilo wakati muafaka na ukishindwa katika mipango
yako kubali kushindwa na anzisha chama chako au kama Ndugu yangu Mabere Marando
jiunge na chama unachokubaliana nacho zaidi ya hicho ulimo.
Haiwezekani eti chama cha
maana kiogope kuondoka kwa wanachama wafuasi wa mwanachama au kiongozi mmoja au
wawili au watatu wanaojiona wao ni bora kuliko wenzao. Kwa kitendo cha Chadema
kuwavua uanachama viongozi wao wanadamizi wanaokiri tena na tena kuwa walisuka
mtandao wa siri wa kuwaondoa katika chaguzi zijazo viongozi wenzao wanaowaona
wao kuwa ni wahafidhina na wao ni wanademokrasia ni kitendo cha ujasiri na
kujenga uhalali wa kudumu wa Chadema hata kama kitayumba na kutorokwa na
wanachama kiasi kidogo au kikubwa kwa sasa na hata kukosa ushindi kwenye
changuzi za wakati huo.
Uchambuzi wenye kusukumwa
na tafakuri tunduizi unanituma niseme heko Chadema kwa kuthubutu hata kama
chama kitashindwa katika uchaguzi wowote ujao. Kitendo hiki pekee kimeonesha
njia kwa kusema kuwa dhana ya "Umoja ni Ushindi" ni dhana bora kuacha
itekelezwe na CCM ya mafisadi ambao kwao kuwa na timu ambayo ina akina Ronaldo
kibao kila mmoja akikimbia na mpira kufunga yeye badala ya kutoa pasi ni jadi
ya CCM ya leo. Lengo ni labda kutafuta kumzidishia umaarufu Ronaldo mhusika binafsi
na labda kwa CCM ya sasa hilo ni sawa kwa vile CCM haijioni kama chama cha
ukombozi tena bali chama dume na chama tawala milele na milele. Chadema ya
Freeman Mbowe, Dakta Slaa, John Mnyika, Mabere Marando, Prof Baregu na Prof
Safari, kutaja wachache, ni bora iendelee kujiona kama chama cha ukombozi kuona
ni sawa kukataa dhana ya ki-CCM ya "Umoja ni Ushindi"
Uchambuzi wangu unaweka
kando urafiki na udugu wa kifamilia wa karibu kati yangu na Dakta kitila Mkumbo
na mwanangu Zitto Kabwe na heshima na mapenzi yangu kwao kama wachambuzi mahiri
wa mambo vinabaki pale pale. Wanaweza kuishi bila hata kuwa kwenye chama
chochote kama mimi na bado wakaendelea kutetea mabadiliko Tanzania katika
nafasi zao katika jamii.

0 comments:
Post a Comment