![]() |
| Ndugu wa wafungwa wakisukumana na maafisa usalama katika jela moja ya mji wa Nuevo Leon. |
KWA uchache wafungwa saba wamepoteza maisha katika jela
moja katika jimbo la kasikazini mashariki la Tamaulipas nchini Mexico.
Kwa mujibu wa maafisa usalama wa jimbo hilo, ambao
walizungumza kwa masharti ya kuficha majina yao, walisema kuwa tukio hilo
lilitokea jana Jumamosi katika gereza moja la mji wa Altamira, kiasi cha
kilomita 480 (maili 300) kusini mwa mpaka wa Mexico na Marekani.
Aidha, maafisa hao walisema kuwa wafungwa hao wenye umri
kuanzia miaka 20 mpaka 50, walipoteza maisha yao katika mapigano yaliyoibuka
ndani ya chumba kimoja cha wafungwa.
Maafisa wa gereza wanasema kuwa wafungwa tisa, waliokuwa
na matatizo na wale waliouawa, ndio walioanza mapambano, ambapo mbali na hao
waliokufa, watu wawili walijeruhiwa na wengine tisa walitiwa nguvuni.
Mwezi Januari 2012, wafungwa 31 walipoteza maisha katika
ghasia zilitokea katika gereza hilo hilo, huku magereza nchini humo yakiendelea
kushuhudia ghasia, vurugu, mauaji na utorokaji wa wafungwa.
Mwezi Desemba 2012, watu 17, wakiwemo askari 6, waliuawa
katika ghasia zilizotokea katika gereza moja katika mji wa Gomez Palacio.
Tukio hilo lilitokea katika jimbo la Durango, wakati
wafungwa walipokuwa wakijaribu kutoroka gerezani na kukimbia kupitia mifereji
ya chini ya gereza hilo.
Mwezi Septemba 2012, zaidi ya wafungwa 130 nchini humo
walitoroka jela iliyokaribu na mpaka wa Marekani kwa kupitia kwenye mfereji wa
maji machafu wa chini ya gereza hilo.
Matukio ya wafungwa kutoroka kwa wingi kutoka magerezani
yamekuwa yakiongezeka katika miaka ya hivi karibuni na maafisa wa magereza
wamekuwa wakilaumiwa kwa kuwa na usuhuba na magenge yanayojihusisha na madawa
ya kulevya.
Tangu mwaka 2010, matukio kadhaa ya utorokaji magerezani
yamekuwa yakiripotiwa kwa wingi sana nchini Mexico. Mwezi Desemba mwaka huo, zaidi
ya wafungwa 140 walitoroka katika gereza moja katika mji wa mpakani wa Nuevo
Laredo katika jimbo la Tamaulipas.

0 comments:
Post a Comment