![]() |
| Kamanda wa Operesheni za jeshi la Kongo katika Jimbo la Kivu Kaskazini, Kanali Mamadou Ndala, akimpa taarifa gavana wa Jimbo la Kivu Kaskazini Julieni Paluku mjini Kibumba. |
VIKOSI vya serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo vimeukamata mji wa Rutshuru katika siku ya tatu ya mapambano makali katika eneo la mashariki mwa nchi hiyo.
Mapigano hayo yalizuka siku ya Ijumaa baada ya
mazungumzo ya amani baina ya serikali na waasi wa M23 kukwama baada ya waasi
kutaka viongozi wao wote wasamehewe kikamilifu bila masharti yoyote.
Jana Jumapili,
msemaji wa jeshi la Kongo, Kanali Olivier Hamuli aliiambia redio ya
Umoja wa Matifa, Okapi, kuwa vikosi vya serikali vimeudhibiti mji wa Rutshuru, kiasi cha kilometa 70 (maili 43) kaskazini mwa mji wa Goma, ambao
ndio mji mkubwa kabisa katika eneo la mashariki mwa Kongo.
Waasi walikuwa wakiudhibiti mji wa Rutshuru tangu mwaka
mmoja uliopita. Walikuwa wakiutumia mjhuo kama ngome yao ya kijeshi ya jimbo.
Mapema Jumapili, jeshi liliukamata mji wa Kiwanja
uliokuwa ukishikiliwa na waasi, siku moja baada ya mapambano makali kwenye mji
muhimu wa Kibumba ambao upo kwenye mpaka wa nchi hiyo na Rwanda.
“Tunaimarisha maeneo tuliyoyachukua,” alisema Hamuli,
huku akikataa kuzungumzia ombi la waasi kutaka kurudi kwenye meza ya
mazungumzo: “Tutaendelea kufanya kazi zetu kama askari.”
KAULI YA M23
Katika taarifa yake ya jana Jumapiili, M23 walisema kuwa
waliyaondoa majeshi yao kutoka mji wa Kiwanja na kulituhumu jeshi la Kongo kuwa
liliwatuma askari wake wakiwa wamevaa nguo za kiraia ili kuwafanya askari wa
Umoja wa Mataifa kuingilia kati.
Kundi hilo pia lilitishia kuwaondoa wajumbe wake kutoka
katika mazungumzo yaliyokwama iwapo hakutakuwa na “usitishwaji wa haraka wa
mapigano.”
ASKARI WA TANZANIA AUAWA
Wakati huo huo, tume ya Umoja wa Mataifa ya kusimamia
amani ya Kongo (MONUSCO) imesema kuwa
askari mmoja wa Tanzania katika kikosi cha kulinda amani aliuawa wakati wa mapambano
na waasi wa M23 katika eneo la Kiwanja.
“Askari huyo alifariki wakati akiwalinda wananchi wa
Kiwanja,” alisema mkuu wa MONUSCO, Martin
Kobler, katika taarifa yake.
Umoja wa Mataifa umetuma brigedi maalumu ya askari 3,000
wa Kiafrika wenye mamlaka ya kupambana nchini Kongo.
Makundi kadhaa yenye silaha, ikiwemo M23, wanaendesha
harakati zao za uasi mashariki mwa Kongo na wanapigania kuidhibiti nchi hiyo
kubwa yenye maliasili za madini, kama vile dhahabu, urani, coltan, ambayo
hutumika katika utengenezaji wa vifaa vingi vya elektroniki, ikiwemo simu za
mkononi.
Waasi wa M23 walijiondoa katika jeshi la Kongo mwezi
Aprili 2012 kupinga kile walichodai kuwa ni mwenendo mbaya ndani ya jeshi la
Taifa (FARDC). Walikuwa wamejumuishwa katika jeshi chini ya mkataba wa amani
uliosainiwa mwaka 2009.
Tangu mwezi Mei 2012, takriban watu milioni 3
wameyekimbia makazi yao katika eneo la mashariki mwa Kongo. Takriban watu
milioni 2.5 ni wakimbizi wa ndani, huku zaidi ya watu 460,000 wamekimbilia
katika nchi za Rwanda na Uganda.
Kongo imekuwa ikikabiliwa na matatizo matatizo kwa
miongo kadhaa, kama vile umaskini uliokithiri, miondombinu mibovu, na vita
katika eneo la mashariki mwa nchi hiyo ambavyo viliibuka tangu mwaka 1998 na
kugharimu maisha ya zaidi ya watu milioni 5.5.

0 comments:
Post a Comment