Viongozi wa dini wametaja majina 61 ya vinara
wanaojihusisha na dawa za kulevya nchini ambao wanatarajia kuwaburuza katika
Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC), mjini The Hague, Uholanzi kujibu tuhuma
zao.
Majina hayo yametajwa na Kamati ya Maadili na Haki za
Jamii kwa Viongozi wa Dini na Wananchi nchini, ambapo miongoni mwao wamo
wabunge wa majimbo na viti maalum, mawaziri, viongozi wa dini na
wafanyabiashara.
Mwenyekiti wa kamati hiyo Mchungaji wa Kanisa la
Kiinjili la Kipendekoste, William Mwamalanga, aliliambia gazeti hili kuwa,
majina hayo yalipatikana Jumanne wiki hii kupitia mkutano wa siri wa viongozi
wa dini wa madhehebu ya kiislam na kikristo 134 kutoka Tanzania Bara, Zanzibar
na Pemba.
Mkutano huo ambao ulifanyika kwa siku mbili kuanzia
Oktoba 21, mwaka huu hapa jijini Dar es Salaam uliwakilishwa na viongozi wawili
wa dini kila mkoa isipokuwa Rukwa ambapo hapakuwa na mwakilishi.
Alisema ulifanyika kwa siri ili kutotoa mwanya wa
kuingiliwa na mifumo isiyo rasmi ambayo ingevuruga adhima yao.
Kuhusu upatikanaji wa majina, mchungaji huyo alisema
ulitokana na utafiti walioufanya ndani na nje ya nchi.
Pia alisema taarifa nyingine walizipata kupitia kwa
wasiri wao kutoka ndani ya jeshi la polisi nchini na vyanzo mbalimbali vya
habari kutoka nje ya nchi.
Akizungumzia mkutano huo, alisema lengo lake lilikuwa ni
kutathmini biashara za dawa hizo ambazo alieleza ni tishio linaloangamiza kwa
kasi kubwa vijana na kusababisha nchi kuingia kwenye aibu duniani.
Mchungaji Mwamalanga alisema katika mkutano huo walitoka
na maazimio mawili likiwamo la kuwafikisha mahakamani wahusika na kufanya
kampeni za siri kupita kwenye majimbo sita ya wabunge (majina tunayo)
waliotajwa.
Alisema lengo la kampeni hiyo ni kuwaeleza wananchi
tabia za wawakilishi wao ili mwaka 2015 waweze kuchagua viongozi bora wenye
uchungu na nchi yao, wakereketwa wa amani na watakaochochea watu kujituma na
kufanya kazi kwa bidii.
Alisema wakati wa uchaguzi mkuu wawakilishi wa mkutano
huo, watapita tena majimboni kuwataja wahusika kwa majina.
Kuhusu viongozi wa dini ambao nao wametajwa kujihusisha
na biashara hiyo, mwenyekiti huyo alisema, mkutano umewataka wafuate mfano wa
Mchungaji Donald Mwakisambwe wa kanisa la Kiinjili la Kipentekoste nchini,
ambaye aliacha kwa ridhaa yake.
Aidha, kamati hiyo imetoa siku 71 kuanzia Jumanne ya
wiki hii kwa wahusika wote 61 kujisalimisha wenyewe kwa Rais Jakaya Kikwete.
“Wakati mchakato wa kuyapeleka majina haya ICC
ukiendelea tunawataka wahusika wajisalimishe kwa Kikwete kwa kuwa orodha hii
tuliyonayo (akitaja majina yao) ni miongoni mwa wale waliotajwa kwenye orodha
aliyokabidhiwa Rais wakati ule, wakijisalimisha tutajua kupitia wasiri wetu,”
alisema na kuongeza:
“Vinara hawa ambao Watanzania wamekuwa wakiwaita ‘vigogo
wa dawa za kulevya’ hawapaswi kuitwa jina hili, hawa ni wahuni na wauaji,
tusiwape majina mazuri ambayo yanawatukuza ndiyo maana biashara hii inakuwa kwa
kasi,” alisema.
Kuhusu Watanzania 175 waliokamatwa nchini China ambao
wanasubiri adhabu ya kunyongwa na wengine waliowahi kukamatwa nchi nyingine
duniani alisema, utafiti waliofanya unaonyesha kuwa wengi wao hutumwa na
wakubwa hapa nchini na kuahidiwa fedha nyingi.
“Tumekubaliana wakati vijana wetu wakisubiri adhabu hiyo
ya kunyongwa basi ICC iwatambue wahuni (vigogo) wanaosababisha biashara hii hapa
Tanzania,” alisema.
Alisema katika mkutano huo wa siri alikuwapo mtaalam wa
sheria mstaafu aliyekuwa akifanya kazi katika mahakama ya ICC ambaye
amewasaidia jinsi ya kufungua kesi hiyo mahakamani hapo.
Aliongeza kuwa, kesi hiyo itaambatanishwa kielelezo cha
asadi ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William
Lukuvi, ambayo aliitoa mwezi Agosti mwaka huu bungeni kwa kusema kuwa hawezi
kuwataja hadharani wabunge waliotajwa kujihusisha na dawa za kulevya.
Katika taarifa ya waziri Lukuvi alisema serikali haiwezi
kuwataja kwa haraka kwa kuwa haina ushahidi kwa kuhofia kushindwa mahakamani.
Mchungaji Mwamalanga alisema maelezo ya Lukuvi kwao ni
ushahidi kuwa, wapo wanaojihusisha na biashara hizo.
Akibainisha miongoni mwa tafiti walizowahi kufanya
katika majimbo nane nchini ambayo ni Dar es Salaam (Kinondoni), Tanga, Mbeya,
Mwanza, Iringa , Dodoma, Lindi, Arusha alisema kila wiki kati ya vijana watano
hadi sita hupoteza maisha kutokana na matumizi ya dawa hizo.
Alisema wilaya ya Kinondoni walibaini tatizo ni kubwa
ambapo ni mara tatu ya idadi hizo hapo huu.
“Utafiti ulibaini asilimia kubwa ya waendesha bodaboda
wamekuwa wakifariki na vyombo vyao kutokana na kujihusisha na matumizi ya dawa
hizi, ukubwa wa tatizo ulionekana kwenye mikoa ya Tanga, Mbeya na Dar es
Salaam,” alisema.
Mwenyekiti huyo, alisema mkutano huo umemtaja Waziri wa
Uchukuzi, Harrison Mwakyembe, kuwa ni waziri aliyefanya vizuri katika mapambano
hayo ambaye amesababisha kwa sasa usafirishwaji wa dawa hizo kwa njia ya viwanja
vya ndege kukoma.
Pia alisema Kamanda wa Polisi Kitengo cha Kuzuia na
Kupambana na Dawa za Kulevya, Geofrey Nzoa, amejitahidi kupambana na tatizo
hilo kwa kuwa muwazi na mwaminifu (kutopokea rushwa).
Katika hatua nyingine, gazeti la NIPASHE limechukua nafasi
ya kwanza katika kuibua na kuzichapisha habari mbalimbali zinazohusu dawa za
kulevya na kusababisha baadhi ya wauzaji kujisalimisha wenyewe.
Mchungaji Mwamalanga alisema nafasi hiyo imekuja kupitia
utafiti wao uliohusisha gazeti tofauti nchini ambapo NIPASHE liliibuka kidedea
baada ya kuonekana mara kwa mara ikitoa taarifa za dawa za kulevya.
“Katika mkutano wageni wetu kutoka nchi ya Kidemokrasia
ya Kongo, walieleza jinsi NIPASHE lilivyosaidia viongozi wao wa dini 14
waliokuwa wakijuhusisha na biashara hiyo, walivyoacha baada ya gazeti hili
kuibua habari mbalimbali,” alisema.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
0 comments:
Post a Comment