![]() |
| Askari wa Kobgo wakisonga mbele katika eneo la mlima Kasanza lililokuwa likishikiliwa na waasi, kaskazini mwa Goma, Oktoba 25, 2013. |
Na Kabuga Kanyegeri
JESHI la serikali ya Kongo likisaidiwa na vikosi vya
Umoja wa Mataifa limeendelea kutoa kipigo kwa waasi wa M23 waliokuwa wakitishia
usalama wa miji ya eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo,
mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini humo amesema.
Martin Kobler, ambaye pia ni mkuu wa Tume ya Umoja wa
Mataifa ya Kusimamia amani ya Kongo (MONUSCO), aliyasema hayo wakati akitoa
taarifa yake kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kupitia mawasiliano ya
video jana Jumatatu.
"Kwa ujumla M23 wameondoka katika maeneo yote jana,
isipokuwa eneo dogo linalopatikana mpakani mwa Rwanda,” alisema.
Kobler alisema kuwa M23 waliondoka katika ngome yao
muhimu kwenye Mlima Hehu jirani na mpaka wa Rwanda, akaongeza kuwa, “Kwa M23
wamefikia mwisho kijeshi.”
Gerard Araud, balozi wa Ufaransa kwenye Umoja wa
Mataifa, ambaye alikuwepo wakati Kobler akitoa taarifa yake, alithibitisha
ripoti hiyo.
"Leo tunaweza kusema kuwa M23 imekwisha kijeshi,” Araud
aliwaambia waandishi wa habari na kusisitiza kuwa “maeneo mengi yaliyokuwa
yakishikiliwa na M23 yamechukuliwa na vikosi vya jeshi la Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo.”
Araud na wanadiplomasia wengine kwenye Umoja wa Mataifa
walielezea matarajio kuwa hatua ya waasi kushindwa kwenye uwanja wa mapambano
kutawashawishi kurudi kwenye meza ya mazungumzo ya amani.
Mazungumzo ya amani kati ya serikali ya Kongo na waasi
wa M23 yamesimama kutokana na kutokubaliana kwenye suala la msamaha kwa
viongozi wa waasi.
Jeshi la Kongo linapambana na waasi kwa msaada wa
brigedi mpya ya Umoja wa Mataifa inayoongozwa na Tanzania ikiwa na mamlaka ya
kupambana. Brigedi hiyo yenye askari 3,000, imepewa nguvu kubwa zaidi kuliko
vikosi vingine vya Umoja wa Mataifa vilivyowahi kutumwa kwenye shughuli za
kulinda amani.
Brigedi hiyo iliundwa baada ya waasi wa M23 kuuvamia na
kuukalia kwa muda mji wa Goma wenye wakazi wapatao milioni moja novemba mwaka
jana. Waasi hao waliondoka katika mji huo Desemba 1,2012 chini ya makubaliano
ya kusitisha mapigano.
Makundi kadhaa yenye silaha, ikiwemo M23, wanaendesha
harakati zao za uasi mashariki mwa Kongo na wanapigania kuidhibiti nchi hiyo
kubwa yenye maliasili za madini, kama vile dhahabu, urani, coltan, ambayo
hutumika katika utengenezaji wa vifaa vingi vya elektroniki, ikiwemo simu za
mkononi.
Waasi wa M23 waliuteka mji wa Goma Novemba 20, 2012
baada ya walinda amani kuondoka katika
mji huo wenye wakazi milioni moja. Wapiganaji wa M23 waliondoka katika mji huo
Desemba 1,2013 baada ya makubaliano ya kusimamisha mapigano.
Waasi wa M23 walijiondoa katika jeshi la Kongo mwezi
Aprili 2012 kupinga kile walichodai kuwa ni mwenendo mbaya ndani ya jeshi la
Taifa (FARDC). Walikuwa wamejumuishwa katika jeshi chini ya mkataba wa amani
uliosainiwa mwaka 2009.
Tangu mwezi Mei 2012, takriban watu milioni 3
wameyekimbia makazi yao katika eneo la mashariki mwa Kongo. Takriban watu
milioni 2.5 ni wakimbizi wa ndani, huku zaidi ya watu 460,000 wamekimbilia
katika nchi za Rwanda na Uganda.
Kongo imekuwa ikikabiliwa na matatizo matatizo kwa
miongo kadhaa, kama vile umaskini uliokithiri, miondombinu mibovu, na vita
katika eneo la mashariki mwa nchi hiyo ambavyo viliibuka tangu mwaka 1998 na
kugharimu maisha ya zaidi ya watu milioni 5.5.

0 comments:
Post a Comment