
Wakati suala la ujasusi unaofanywa na Marekani kwa mawasiliano
ya viongozi na mamilioni ya watu wengine duniani kote likiwa linaitikisa
Jumuiya ya Umoja wa Ulaya, ripoti mpya iliyochapishwa hivi karibuni imeonesha
kuwa Marekani imekuwa ikiyamulika mawasiliano ya simu ya Kansela wa Ujerumani,
Angela Markel tangu mwaka 2002.
Gazeti la kila wiki la nchini Ujerumani, Der Spiegel,
limesema katika ripoti iliyochapishwa jana kuwa liliona nyaraka za siri kutoka
Shirika la Usalama la Marekani (NSA) zinazoonesha kuwa simu ya mkononi ya
Merkel iliwekwa katika orodha maalumu inayofuatiliwa na Shirika hilo tangu
mwaka 2002.
Ripoti hiyo imeongeza kuwa mwezi Juni 2013 namba ya simu
ya mkononi ya kansela huyo wa Ujerumani bado ilikuwa katika orodha ya simu
zinazopekuliwa na shirika hilo.
Maepna Ijumaa, serikali ya Ujerumani ilisema kuwa wakuu
wake wa usalama wangetembelea Washington mapema ili kuchunguza sakata hilo.
Msemaji wa serikali hiyo, Georg Streiter, amesema kuwa
wakuu wa ujasusi wa ndani na nje watakutana na maafisa mbalimbali kutoka Ikulu
ya Marekani na wale wa NSA.
Wakati huo huo, msemaji wa Shirika la Usalama la
Marekani, Caitlin Hayden alisema kuwa Wajerumani hao watakaribishwa, lakini
hakueleza kwa undani zaidi ni kwa jinsi gani Washington itashughulikia ghadhabu
iliyooneshwa na Wajerumani dhidi ya vitendo vya kurikodi mazungumzo ya viongozi
wake.
Siku ya Alhamisi, gazeti la The Guardian liliripoti kuwa
NSA ilirikodi mazungumzo ya simu za viongozi 35 wa mataifa mbalimbali.
Snowden, mfanyakazi wa zamani wa CIA, alivujisha
programu kubwa mbili za siri mno kutoka serikali ya Marekani zinazotekelezwa na
NSA na FBI, ambapo huzifanyia ujasusi na kurikodi mamilioni ya simu za wananchi
wa Marekani na wale wa Ulaya na kutega taarifa za mawasiliano ya intaneti
kutoka kwenye makampuni makubwa ya mitandao kama vile Facebook, Yahoo, Google,
Apple, na Microsoft.
Sakata la NSA lilifumuka zaidi baada ya Snowden kufichua
taarifa za Marekani kuzifanyia ujasusi nchi rafiki.
0 comments:
Post a Comment