Mahakama ya Wilaya Singida imewahukumu watu wanne
kutumikia vifungo vya miaka 120 jela kwa kuteka gari lililokuwa likisafirisha
maiti kutoka mkoani Morogoro kwenda Musoma mkoani Mara na kupora waombolezaji
kompyuta na fedha.
Waliohukumiwa vifungo hivyo kila mmoja miaka 30 jela ni
Hamis Ali (23), Hamisi Issa (33); Khaldi
Hamis (21) na Abubakari Jumanne (26), wakazi wa Kisaki Manispaa ya Singida.
Mshtakiwa wa kwanza Iddi Omari (38), aliachiwa huru
baada ya mahakama hiyo kukosa ushahidi
wa kumtia hatiani. Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Flora
Ndale, alisema ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka bila kuacha shaka
umethibitisha washtakiwa hao walitenda kosa hilo.
Awali, Mwendesha Mashtaka,Sajini, Godwel Lawrence,
alidai kuwa Desemba 6, mwaka 2012, saa
7:30 mchana, eneo la Kisaki, washtakiwa hao waliteka gari lenye namba za
usajili SU 37012 aina ya Toyota Land Cruiser mali ya serikali lililokuwa
likiendeshwa na Kalistus Malipula, wakati limebeba mwili wa Munchari Lyoba
aliyefariki dunia akiwa mwanafunzi mwaka wa tatu Chuo Kikuu cha Kilimo
Sokoine (Sua) kwa ajili ya kuusafirisha
kutoka Morogoro kwenda Musoma mkoani Mara kwa maziko
Alidai baada ya washtakiwa hao kuteka gari hilo
waliwapora waombolezaji vitu mbalimbali zikiwamo kompyuta mpakato, simu za
mkononi na fedha taslim zaidi ya Sh. milioni 8.7.
Alidai pia walivunja jeneza na kuufanyia upekuzi mwili
wa marehemu huyo kwa kuchana sanda wakidhani kulikuwa na fedha zilizofichwa.
Kwa upande wao,
washtakiwa hao waliiomba mahakama iwapunguzie adhabu kutokana na
kutofanya kosa hilo, umri wao kuwa mdogo na wanategemewa na familia zao.
Ombi hilo lilipingwa na mwendesha mashtaka na kuiomba
mahakama kutoa adhabu kali ili liwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama
hiyo.
Hakimu Ndale alisema kosa lililofanywa na washtakiwa hao
ni la kinyama na lisingeweza kuvumilika katika jamii, hivyo ili liwe fundisho
kwa wote wanaofikiria kufanya vitendo vya kinyama kama hicho, anawahukumu kila
mmoja kutumikia kifungo cha miaka 30 jela.
CHANZO: NIPASHE
0 comments:
Post a Comment