
Watu sita wamefariki dunia na wengine 34 kujeruhiwa
katika ajali ya barabarani iliyotokea eneo la Chinangali wilayani Chamwino
mkoani Dodoma baada ya basi la kampuni ya Al Sayeed lililokuwa likitokea jijini
Dar-Es-Salaam kwenda Dodoma kugongana uso kwa uso na lori la mizigo lililobeba
shehena ya mahindi likitokea Dodoma kwenda Dar es salaam.
Akithibitisha kutokea kwa ajali hiyo kaimu kamanda wa
polisi mkoa wa Dodoma Mrakibu Mwandamizi Damas Nyanda amesema chanzo cha ajali
hiyo ni mwendo kasi wa dereva wa basi hilo lenye namba za usajili T 433 BLR
aina ya Youtong ambaye alishindwa kulimudu na kuacha njia na kulivaa lori aina
ya Layland Daf lenye namba za usajili T 102 CGR likiwa na tela lenye namba za T
928 na kusababisha watu watano kufariki papo hapo.
ITV ilifika katika eneo la tukio na kuzungumza na baadhi
ya mashuhuda wa ajali hiyo na wamelalamikia uhaba wa vyombo vya uokoaji ambapo
wamesema kama vyombo vya uokoaji vingefika kwa wakati huenda watu wote wanne
waliofariki kwenye lori wangeokolewa.
Nao baadhi ya majeruhi waliolazwa katika hosipitali ya
rufaa ya Dodoma wamesema kabla ya kutokea kwa ajali hiyo dereva wa basi hilo
alikuwa katika mwendo kasi na baada ya kuliona lori hilo alifunga breki za
ghafla na kusababisha basi hilo kulivaa lori hilo huku mganga mfawidhi wa
hosipitali hiyo Dk Mzee Nasoro akasema walipokea majeruhi 20 na mmoja kati yao
amefariki dunia.
CHANZO: ITV
0 comments:
Post a Comment