![]() |
| Balozi wa China nchini, Dk. Youging (kulia) akiwa kwenye mkutano wa CCM.(Kushoto) Nape Nnauye na Abdulrahman Kinana. (katikati) |
Balozi wa China nchini, Dk. Lu Youqing, ameibuka na
kusema kuwa msichana asiyemfahamu ndiye aliyemvisha kofia ya Chama Cha
Mapinduzi (CCM) kwa nguvu wakati akiwasalimia wananchi wa Mkoa wa Shinyanga
katika mkutano wa hadhara wa chama hicho tawala.
Balozi huyo alisimama jukwaani takribani wiki mbili
zilizopita katika moja ya mikutano iliyohutubiwa na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana pamoja na Katibu Mwenezi
wa chama hicho, Nape Nnauye, katika wilaya za Kishapu na Shinyanga Mjini.
Aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati
akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya uwekaji saini mkataba wa
ushirikiano wa kibiashara kati ya Mfuko wa Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) na
Baraza la Wafanyabiashara wa watu wa China Tanzania (CBCT).
Alisema alikwenda mkoani Shinyanga kwa shughuli za
kiserikali kuwahamasisha wananchi wa mkoa huo kulima zaidi pamba na siyo
mwaliko wa CCM kama inavyotafsiriwa na baadhi ya watu.
Balozi Youqing alisema alipokuwa katika mkutano huo wilayani Kishapu, alipewa nafasi ya
kuwasalimia wananchi wa mkoa huo na kuwahamasisha juu ya ulimaji wa pamba.
Alisema mara baada ya kupanda jukwaani ghafla alitokea
msichana asiyemfahamu wala kumkumbuka aliyemvua kofia yake na kumvika ya CCM
kwa nguvu.
Alieleza kuwa alijaribu kumzuia msichana huyo, lakini
alishindwa.
“Alikuja msichana mmoja mrembo, ghafla wakati nikiwa
jukwaani, nilijaribu kumzuia kunivua kofia yangu, lakini nilishindwa, alitumia
nguvu,” alisema Youqing.
Alisema hakuna mtu yeyote hapa nchini atakayeweza
kumzuia balozi wa China kufanya vitu vizuri vyenye faida kwa Watanzania na
Taifa kwa ujumla.
Alisema hakujua kama kitendo kile kingetafsiriwa vibaya
na wananchi wa Tanzania, na kueleza kuwa hakujua kama Watanzania wangekasirika
kwa kuwa anaamini Watanzania wote ni kitu kimoja. Balozi huyo alisema yupo
tayari kufanya kazi na chama chochote cha siasa nchini alimradi sheria na
taratibu zifuatwe.
Hatua ya balozi huyo kuvaa kofia ya CCM ililalamikiwa na
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Septemba 16, mwaka huu kupitia kwa
Mkurugenzi wa Mambo ya Nje, Ezekia Wenje, aliyesema kitendo cha Balozi Youqing
kilikiuka mkataba wa Vienna wa mwaka 1961.
Wenje alisema kuwa kutokana na hali hiyo, Chadema
kitaiandikia Serikali ya Tanzania, Umoja wa Mataifa na Serikali ya China
kuwasilisha malalamiko dhidi ya Balozi
Youqing.
Chama hicho kiliongeza kuwa kisingependa uhusiano wa
kihistoria kati ya China na Tanzania ambao umedumu kwa muda mrefu tangu Uhuru
uingizwe matatani au shakani kwa sababu ya mapenzi binafsi ya balozi kwa CCM.
Siku hiyo hiyo, Septemba 16, mwaka huu, serikali kupitia
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, ilisema kuwa
kitendo kilichofanywa na Balozi huyo siyo sahihi na kinakiuka mkataba wa
Vienna.
Membe alisema kitendo cha Balozi yeyote kuhudhuria
mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa na kuvaa sare zenye nembo ya vyama vya
siasa siyo sahihi na kinakiuka Kifungu cha 41(1) cha Mkataba wa Vienna wa mwaka
1961, unaoongoza uhusiano wa kidiplomasia.
Taarifa ya Waziri Membe ilieleza kuwa mkataba huo
unazuia wawakilishi wa nchi za nje kujihusisha na ushabiki wa kisiasa
wanapofanya kazi zao kwenye nchi za uwakilishi.
Alisema katika kipindi cha mwaka 2010 hadi 2012, Wizara
ilikumbana na vitendo vinavyofanana na kitendo hiki na ikachukua hatua stahiki
na kwamba kwa tukio hilo la Balozi wa China, Wizara itachukua hatua za
kidiplomasia zinazostahili ili kuzuia jambo hilo lisitokee tena.
Msajili wa Vyama Vya Siasa, Jaji Francis Mutungi,
Alhamisi iliyopita alikemea kitendo cha CCM kumshirikisha Balozi Youqing,
katika shughuli zake za kisiasa.
Alisema tukio
hilo ambalo CCM kiliruhusu raia wa kigeni kutumia jukwaa lake, ni dhahiri
limezua hali ya taharuki kwa wananchi na kwamba Sheria ya vyama vya Siasa kwa
upande wake iko kimya katika suala hilo.
Jaji Mutungi alisema Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa
inaunga mkono kwa dhati kabisa hatua iliyochukuliwa na Wizara ya Mambo ya Nje
na Ushirikiano wa Kimataifa, kukemea jambo hilo na kwamba tamko la serikali
limezingatia sheria na wajibu wa wanadiplomasia wakati wa uwapo wao nchini.
Jaji Mutungi alisema kama mlezi wa vyama vya siasa,
anavitaka vyama hivyo kuzingatia na kufuata sheria na taratibu stahiki katika
utekelezaji wa shughuli zao za kisiasa.
Alisema kuwa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kwa
sasa ipo kwenye mchakato wa marekebisho ya Sheria husika ya Vyama vya Siasa
ambayo imebainika kuwa na upungufu na lengo ni kukabiliana na changamoto
zilizopo ikiwamo suala hili lililojitokeza.
AZUNGUMZIA WACHINA KUTISHWA
Katika hatua nyingine, Balozi Youqing alizungumzia madai
ya kuandikiwa barua na Mtanzania mmoja anayejitambulisha kama Kamanda wa CCM
Asilia alitaka Wachina wote waondoke nchini kabla ya kuanza kuuawa kutokana na
balozi wao kushabikia CCM na Wachina kujihusisha na uhalifu, na kusema kuwa
anaamini Tanzania ina sheria na taratibu zinazozuia mtu kuvunja sheria.
Hivyo kama kuna atakayebainika kufanya kitendo hicho,
sheria itachukua mkondo wake.
Alisema kitendo
chochote cha uvunjifu wa amani kinachoweza kutokea hapa nchini anaamini Jeshi
la Polisi litapambana nalo. Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI),
Kamishna Robert Manumba, alipotafutwa kuelezea tukio hilo la raia wa China
kutishiwa kuuawa, alisema Polisi bado wanachunguza.
“Vijana wangu bado wanafuatilia hilo suala, wapo
kazini,” alisema Manumba.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:
Post a Comment