MAHAKAMA moja ya kijeshi nchini Misri imewahukumu wanachama 11 wa vuguvugu la Udugu wa Kiislamu kifungo cha maisha jela katika wakati ambao serikali ya nchi hiyo inaendeleza mapambano dhidi ya kundi hilo lenye nguvu zaidi kisiasa kuliko makundi yote nchini humo.
Watu hao walihukumiwa adhabu hiyo leo kwa tuhuma za “kufyatua risasi na kufanya ghasia” dhidi ya jeshi katika mji wa bandari wa Suez mnano Agosti 14.
Aidha, mahakama hiyo iliwahukumu kifungo cha miaka 5 wafuasi wengine 45 wa vuguvugu hilo huku washitakiwa wengine 8 wakiachiliwa huru.
Ghasia zilizuka katika mitaa ya mji wa Cairo kufuatia hatua ya jeshi kupambana na wafuasi wa rais aliyeondolewa madarakani, Muhammad Mursi.
Mnamo Julai 3, jeshi lilimuondosha madarakani rais aliyechaguliwa kidemokrasia na kumtangaza mkuu wa Mahakama ya Katiba, Adly Mahmoud Mansour, kuwa rais wa mpito. Vilevile, jeshi lilisimamisha matumizi ya katiba na kulivunja Bunge.
Serikali hiyo iliyochaguliwa na jeshi imekuwa ikipambana vikali na wafuasi wa Mursi na imewatia nguvuni wanachama wapatao 2,000 wa vuguvugu la Udugu wa Kiislamu.
Jana Jumatatu, jopo la ushauri la mahakama lililowekwa na serikali hiyo lilitoa shutuma dhidi ya vuguvugu hilo kuwa linakiuka sheria.
Aidha, jopo hilo lliliishauri serikali kulivunjilia mbali vuguvugu hilo, lililosajiliwa kama taasisi isiyokuwa ya Kiserikali (N.G.O).
Hatua hiyo inakuja muda mfupi baada ya kukamatwa kwa kiongozi mkuu wa vuguvugu hilo, Muhammad Badie, mnamo Agosti 20 kwa tuhuma za “kuhamasisha vurugu.”
Badie aliwahi kusema kuwa mapinduzi dhidi ya Mursi yalikuwa batili na kuapa “kuendeleza mapinduzi” yaliyomng’oa mtawala wa zamani wa nchi hiyo, Husni Mubarak mwaka 2011.
Takriban watu 1,000 waliuawa katika ghasia zilizodumu kwa wiki moja baina ya waandamanaji wanaopinga maandamano na vikosi vya usalama baada ya polisi kuzivunja kambi za wanaandamanaji hao mjini Cairo mnamo Agosti 14.
Mauaji hayo yaliibua lawama za kimataifa na kuzifanya taasisi za kimataifa kutoa wito wa kufanyika kwa uchunguzi huru juu ya ghasia hizo.

0 comments:
Post a Comment