Israeli imesema kuwa imefanikiwa kufanya jaribio la makombora kwa kushirikiana na Marekani katika Bahari ya Mediterania, wakati ambapo wasiwasi umetanda katika eneo la Mashariki ya Kati kuhusu uwezekano wa kufanyika mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Syria.
Kwa mujibu wa Wizara ya Masuala ya Kijeshi ya Israeli, makombora aina ya Ankor yalifyatuliwa leo Jumanne katika jaribio hilo kwa kushirikiana na Marekani.
Vyombo vya habari vya Israeli vinasema kuwa kombora hilo lilifyatuliwa katika kuyajaribu makombora ya masafa kama vile Shahab na Scud.
Hayo yanatokea katika hali ambayo jeshi la maji la Marekani linasema kuwa halikufywatua makombora yoyote.
Mapema leo Mzizima 24 iliripoti taarifa iliyotolewa na Wizara ya Ulinzi ya Urusi kuwa rada zake zilibaini kufyatuliwa kwa makombora mawili kutoka katikati mwa Bahari ya Mediterania kwenda upande wa mashariki.
Tukio hilo liligunduliwa na rada za Urusi zilizopo katika mji wa mashariki wa nchi hiyo, Armavir, saa 4:16 asubuhi kwa majira ya Moscow.
Wasiwasi unazidi kuongezeka wakati huu ambapo Marekani inahamasisha kuchukuliwa kwa hatua za kijeshi dhidi ya Syria kutokana na serikali ya nchi hiyo kuhumiwa kuwa ilitumia silaha za sumu katika vitongoji vya mji wa Damascus mapema Agosti 21.
Serikali ya Damascus imekuwa ikikanusha vikali madai hayo na kusema kuwa shambulizi hilo la silaha za sumu lilitekelezwa na waasi kama sehemu ya mkakati wao wa kimapambano uliolenga kuitia hatiani serikali hiyo.
Syria imekuwa katika machafuko makubwa tangu mwaka 2011. Kwa mujibu wa ripoti mbalimbali, nchi za Magharibi pamoja na washirika wao wa Mashariki ya Kati hususan Qatar, Saudi Arabia, na Uturuki, wanadaiwa kuwaunga mkono waasi wa Syria.
Mnamo Julai Julai 25, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon alisema kuwa zaidi ya watu 100,000 wameuawa nchini Syria tangu kutokea kwa machafuko nchini humo.
0 comments:
Post a Comment