
Wizara ya Ulinzi ya Urusi imesema kuwa rada zake zimenasa harakati za makombora mawili yaliyorushwa kutoka katikati ya bahari ya Mediterrania kuelekea upande wa mashariki, yaani Syria.
Hata hivyo, ubalozi wa Urusi nchini Syria umesema kuwa hakuna dalili za shambulio la kombora lililotua mjini Damascus.
Tukio hilo liligunduliwa na rada za Urusi zilizopo katika mji wa mashariki wa nchi hiyo, Armavir, saa 4:16 asubuhi kwa majira ya Moscow.
Duru za kidiplomasia kutoka Damascus zinasema kuwa makombora hayo yaliangukia baharini.
Adiha, ubalozi wa Urusi nchini humo ulieleza kuwa hapakuwepo na dalili za shambulizi la makombora mjini Damascus.
Mnamo Agosti 21, waasi pamoja na makundi ya upinzani nchini humo walidai kuwa watu wapatao 1,300 walipoteza maisha katika shambuli la silaha za sumu lililotekelezwa na serikali katika viunga vya mji wa Damascus vya Ain Tarma, Zamalka na Jobar.
Mataifa kadhaa kama vile Marekani, Ufaransa na Uingereza yalitaka kuchukuliwa kwa hatua ya kijeshi dhidi ya Syria licha ya serikali ya nchi hiyo kukanusha vikali kuhusika kwa vyovyote na shambulizi hilo la sumu.
Mnamo Jumanne, Agosti 27, hali ilizidi kujidhihirisha kuwa kuna uwezekano mkubwa wa kuchukuliwa kwa hatua hiyo. Vyombo vya habari viliripoti kuwa Marekani ilikuwa ikipanga kufanya shambulizi makini, ambalo lingetumia makombora na lingetekelezwa na manowari za kivita kutokea katika bahari ya Mediterania. Ilielezwa kuwa mpango huo ulikuwa ukisubiri idhini na amri ya Rais Barack Obama.
Hata hivyo, baadaye wito mbalimbali kutoka ndani na nje ya Marekani ulizidi kutolewa ukipinga vita ambavyo vilionekana kuzilazimisha baadhi ya nchi zilizopendelea vita kubadili misimamo yao.
Mnamo Agosti 29, Bunge la Uingereza lilipinga ushiriki wa Uingereza, ambaye ni muitifaki mkubwa wa Marekani, katika hatua yoyote ya kijeshi dhidi ya Syria. Wakati serikali ya Uingereza ikijiandaa kutaka idhini ya Bunge kwa mara ya pili, iliamua kuachana na mpango huo tarehe 2 Septemba, ikisema kuwa Bunge limeshazungumza, na kwamba serikali haina mpango wa kurejea tena Bungeni kuomba idhidi ya kushiriki katika vita hivyo.
Mnamo Ijumaa, Agosti 30, Umoja wa Kujihami wa nchi za Magharibi, NATO, nao ulijitenga na kujiweka mbali dhidi ya kushiriki katika vita nchini Syria, huku Katibu Mkuu wa Umoja huo, Anders Fogh Rasmussen, akisema kuwa haoni kama NATO itaingia vitani nchini Syria.
Marekani imeendelea kushikilia msimamo wake, ikisema kuwa inataka kuendelea na mipango yake ya kuishambulia Syria bila kusubiri kibali cha Umoja wa Mataifa au bila hata usaidizi wa waitifaki wake. Hata hivyo, Jumamosi tarehe 31 Agosti, Rais Obama alisema kuwa utawala wake utaanza kuomba idhini ya Bunge la Congress la nchi hiyo ndipo aingize majeshi yake vitani.
Wakati Marekani na Uingereza kwa sasa zinaonekana kusita kuingia vitani, Ufaransa imekuwa ikitaka kufanyika kwa shambulizi la kijeshi dhidi ya serikali ya Assad na kutoa “ushahidi” kuwa serikali ya Syria ilihusika na shambulizi la silaha za sumu lililofanyika Agosti 21. Jana Jumatatu Waziri Mkuu wa Ufaransa, Jean-Marc Ayrault, alisema kuwa, “Ufaransa haitachukua hatua peke yake. Rais anaendelea kuwashawishi washirika wengine kuungana pamoja bila kuchelewa.”
Hili linakuja licha ya maonyo kutoka Umoja wa Mataifa, Urusi, China na Iran dhidi ya hatua hiyo.
0 comments:
Post a Comment