*Mchungaji, waumini sita watiwa mbaroni
*Wageuza makanisa maficho, Uhamiaji yahaha
MSAKO wa wahamiaji haramu umeingia katika sura mpya,
baada ya Idara Uhamiaji Mkoa wa Dar es Salaam, kuanzisha msako mkali katika
nyumba za ibada. Kabla ya kuanzisha msako huo, kumekuwa na taarifa nyingi kuwa
baadhi ya makanisa, hasa ya Pentekoste, yanadaiwa kuhifadhi wahamiaji haramu
kinyume cha sheria.
Katika msako huo, idara hiyo imemkamata Mchungaji wa
Kanisa la Kimataifa la Life Changer Chapel, lililopo Sinza ‘E’, Grace Dangana
Omotok, ambaye ni raia wa Nigeria.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Ofisa Uhamiaji wa Mkoa wa
Dar es Salaam, Grace Hokororo, alisema Mchungaji Grace alikamatwa baada ya
kukiuka masharti ya kibali chake ambacho hakimruhusu kumuingiza raia yeyote
nchini.
Alisema mchungaji huyo, alikamatwa Jumatano wiki hii,
akiwa na raia wengine sita ambao wanaishi nchini kinyume cha sheria.
“Mchungaji Grace ana kibali Class C ambacho hakimruhusu
kuingiza raia wa nchi nyingine.
“Tumekuwa na msako mkali, katika kanisa lake
tumewakamata wahamiaji haramu sita ambao ni raia wa Nigeria na hatujui
aliwaingizaje, tunaendelea na mahojiano nao ili kujua walivyoingia nchini.”
Alisema Idara ya Uhamiaji haina mpango wa kukutana na
viongozi wa dini kuzungumzia uendeshaji wa operesheni hiyo, kwa sababu baadhi
ya viongozi si waaminifu.
“Hatufikiri kukutana na kiongozi yeyote wa dini,
tutaendeleza msako hadi Jiji la Dar es Salaam liwe na wahamiaji halali tu.
“Mfano wa mchungaji huyu, umeonyesha picha ya wazi kuwa
viongozi wa dini si waaminifu, hatuna sababu ya kuzungumza nao, unadhani
watatuambia nini zaidi ya kujitetea?
“Kama kiongozi wa dini alifanya hivyo kwa kupitiwa,
aliposikia kuna msako kwanini asijisalimishe na watu wake?” alihoji Hokororo.
Hata hivyo, alisema nguvu kubwa hivi sasa itaelekezwa
kwenye nyumba za ibada na kwenye saluni mbalimbali jijini humo, maeneo ambayo
yanadaiwa kuwa na wahamiaji haramu wengi.
“Tukipata taarifa kuwa kuna kanisa linawahifadhi
wahamiaji haramu tutafuatilia, huu msako ni endelevu, hata wakijificha wapi
tutawakamata tu,” alisisitiza ofisa huyo.
Alisema wahamiaji haramu ambao watajisalimisha wenyewe
watapewa nafasi ya kusikilizwa kuliko watakaokamatwa katika msako.
Inadaiwa makanisa mengi yanahifadhi wahamiaji haramu kwa
kigezo cha kutangaza neno la Mungu, wakiamini kuwa maeneo hayo ni salama.
Wahamiaji haramu 465 kutoka mataifa mbalimbali,
walikamatwa jijini Dar es Salaam hivi karibuni.
Taarifa za idara hiyo, zinasema kuwa idadi kubwa ya
wahamiaji waliokamatwa ni vijana.
Msako huo, ni utekelezaji wa agizo la Rais Jakaya
Kikwete, alilolitoa Julai 26, mwaka huu, mkoani Kagera, ambapo aliwataka
wahamiaji haramu kuondoka nchini kwa hiari yao.
Wahamiaji kutoka mataifa 17, walikamatwa katika maeneo
mbalimbali mkoani Dar es Salaam.

0 comments:
Post a Comment