* Wamo maofisa wa serikali, wafanyabiashara
* Watakaokamatwa
sasa kufilisiwa mali zao
Serikali imesema miongoni mwa wanaokwamisha vita dhidi
ya ujangili ni wabunge kutokana na baadhi yao kujihusisha na biashara ya pembe
za ndovu.
Pamoja na kuwataja wabunge ambao ndiyo watunga sheria
nchini, serikali imesema pia vita hiyo inashindwa kupata mafanikio kutokana na
kuwa na mtandao mkubwa wa wafanyabiashara wakubwa na maofisa wa serikali
kujihusisha na biashara hiyo.
Hata hivyo, serikali kupitia kwa Naibu Waziri wa
Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, ambaye pia ni Mbunge wa Singida Kaskazini
(CCM), haikueleza ni jinsi gani wabunge wanavyojihusisha na biashara ya pembe
za ndovu ambayo imelalamikiwa sana kutokana na kusababisha idadi kubwa ya tembo
kuuawa katika Hifadhi za Taifa na Mapori ya Akiba.
Baadhi ya maofisa hao wa serikali wametajwa ni pamoja na wa viwanja vya ndege, idara za
wanyama pori na askari wa Jeshi la Polisi.
Nyalandu aliyasema hayo jana muda mfupi baada ya kupokea
maandamano ya wanaharakati wa African Wildlife Trust, ambao walitembea kutoka
mkoani Arusha mpaka jijini Dar es Salaam kwa lengo la kupinga ujangili dhidi ya
tembo.
Nyalandu alisema watu wanaojihusisha na biashara hiyo,
wana mawasiliano ya kisasa.
Alisema mbali na kuwa na mawasiliano ya aina hiyo, pia
wanawatumia vijana ambao huwapa magari na vitendea kazi, zikiwamo silaha za
moto.
Alisema vitu vingine ambavyo vimekuwa vikiikwamisha
serikali kupambana na ujangili, ni rushwa na mmomonyoko wa maadili.
Alisema baadhi ya watumishi wa umma wanaojihusisha na
ujangili wamekuwa wakifanya hivyo kutokana na kusukumwa na uroho wa kutaka
utajiri wa haraka.
Kwa mujibu wa Nyalandu, kumekuwa na ongezeko kubwa la
bei katika biashara hiyo kwenye masoko haramu yaliyoko Mashariki ya Kati ya
Asia, kama China, ikiwa ni pamoja na kuimarika kwa makundi ya majangili.
Alisema kudorora kwa uchumi na ongezeko la umaskini,
kumekuwa kukisababisha watu kuwa na fikra potofu na kujiingiza kwenye vitendo
vya ujangili na kufanya kama sehemu ya kazi yao.
Nyalandu alisema kiwango cha kuuawa kwa tembo imekuwa
ikiongezeka mwaka hadi mwaka.
Alisema mwaka 2009, tembo walikuwa 350,000 na mwaka 2010
hadi 2012, walipungua na kufikia 130,000, huku mwaka huu wakiwa 378 waliouawa.
Aliwataka majangili na wafanyabiashara wanaojihusisha na biashara hiyo kuacha
na kujisalimisha polisi.
Pia alivitaka vyombo vya usalama kushirikiana kwa pamoja
na kwamba majangili hao wakikamatwa watatangazwa katika vyombo vya habari
duniani kote, kupelekwa mahakamani na kutaifisha mali zao.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili
na Mazingira, James Lembeli, alisema idadi ya tembo imepungua sana katika mbuga
za wanyama nchini, hali ambayo imefanya idadi sahihi ya tembo waliobaki
kutojulikana.
Lembeli ambaye pia ni Mbunge wa Kahama (CCM), alisema
serikali lazima isimamie kwa umakini na si kusubiri kukaa barabarani.
Hivyo, alisema kuna haja ya kwenda kwenye mapori walipo
majangili na kupambana nao ili kuepusha tembo kuendelea kuuawa kwani wanyama
hao wanahitajika hasa katika suala zima la kivutio. Lembeli alisema gari la Wizara ya Elimu na
Mafunzo ya Ufundi hivi karibuni lilikamatwa likiwa na pembe za ndovu,
lakini cha kushangaza dereva ambaye alikamatwa aliachiwa baada ya kukaa
siku nne mahabusu ya polisi.
Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Philip Mulugo, alipotakiwa
na NIPASHE jana kuzungumzia suala hilo, aliahidi kulifuatilia.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:
Post a Comment