
WAKATI serikali ya Tanzania ikiendelea na operesheni ya
kuwarejesha makwao wahamiaji haramu, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia
Wakimbizi (UNHCR), limedai kuwa raia hao wamenyanyaswa.
Kwa mujibu wa taarifa ya shirika hilo iliyochapishwa na
Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), takriban wakimbizi 25,000 kutoka
Burundi wameondoshwa Tanzania kwa nguvu katika mwezi mmoja uliopita.
Afisa wa shirika hilo, alisema kuwa malori
yanayowasafirisha Warundi hao yamekuwa yakivuka mpaka kila siku, huku wengi wao
wakikosa maji na chakula.
Kwa sasa Tanzania iko kwenye operesheni ya kuwafukuza
wahamiaji waliojipenyeza nchini bila kufuata utaratibu wa kupata vibali halali.
Mpaka sasa raia wengi wa mataifa mbalimbali wamekamatwa
na kurudishwa makwao huku nchini za Burundi, Rwanda na Jamuhuri ya Kidemokrasi
ya Kongo zikiongoza kwa idadi ya watu.
Kwa miaka mingi Tanzania iliwahifadhi mamilioni ya
wakimbizi waliokuwa wakiyakimbia mapigano katika nchi jirani.
Takriban watu milioni moja walitoroka kutoka Burundi na
kuingia Tanzania wakati wa mgogoro wa wenyewe kwa wenyewe wakati vita
vilipozuka mwaka 1993.
Wengi walirejea kwa hiari wakati amani ilipopatikana
mwaka 2006.
0 comments:
Post a Comment