Jaji wa mahakama moja katika mji wa New Delhi nchini
India ametoa hukumu ya adhabu ya kifo kwa wanaume wanne waliokutwa na hatia ya
kumbaka mwanafunzi wa kike mwenye umri wa miaka 23 kwenye basi mwaka jana.
Watu hao walikutwa na hatia ya kumbaka binti huyo mwezi
Desemba 2012 kwenye gari iliyokuwa
ikitembea katika mji mkuu wa nchi hiyo na kumjeruhi vibaya sana, hali
iliyompelekea kufariki dunia wiki mbili baadaye.
Mshitakiwa mwenye umri mdogo zaidi, ambaye alishitakiwa
katika kesi hiyo, ameshahukumiwa adhabu ya kifungo cha miaka mitatu na kuwekwa
katika jela maalumu ya watoto, huku mshitakiwa wa tano akijinyonga gerezani
mwezi Machi.
Binti huyo amekuwa alama ya hatari zinazowakabili
wanawake nchini India ambapo tukio moja la ubakaji huripotiwa kila baada ya
dakika 21.
Unyama huo uliamsha moto wa hasira na maandamano
yaliyoitikisa nchi nzima na kuilazimisha serikali kuweka sheria maalumu juu ya
usalama wa wanawake.
Katika miaka ya hivi karibuni, India imekuwa na mwenendo
tofauti kuhusu adhabu ya kifo.
Mahakama za India hutoa adhabu za vifo zipatazo 130 kila
mwaka, lakini ni watu watatu pekee ndio walionyongwa ndani ya miaka 17.

0 comments:
Post a Comment