.jpg)
WATU watatu wa familia moja jijini hapa, akiwemo mtoto
wa mwaka mmoja, wameuawa kwa kunyongwa, kukatwa mapanga kichwani na kuchinjwa
mithili ya kuku.
Mauaji hayo yamefanyika kati ya saa 9 na 10 usiku wa
kuamkia jana, katika Kijiji cha Ihyila, Kata ya Buhongwa.
Waliofikwa na mauti hayo ni baba wa familia, Jones Elias
Luhinga (44), mama wa familia, Lusia Elias Luhinga (35), na mtoto Eliud Elias
Luhinga (mwaka mmoja).
Inadaiwa mauaji hayo yametekelezwa na mtu mmoja fundi wa
kujenga nyumba (jina linahifadhiwa kwa sasa), aliyekaribishwa siku tisa
zilizopita na Jones.
Kwa mujibu wa maelezo ya baadhi ya majirani na ndugu wa
familia hiyo ya marehemu, mtu huyo alifanya unyama huo usiku wa manane, na
kwamba alfajiri alioga kisha kuwafungia ndani watoto wengine waliokuwa wamelala
na kutokomea kusikojulikana.
Mmoja wa ndugu wa marehemu Jones, aliyejitambulisha kwa
jina la Benjamin Luhinga aliiambia Tanzania Daima Jumapili kuwa ndugu yake
aliuawa kwa kuchinjwa kama kuku, kisha kukatwa panga katikati ya kichwa na
upande mmoja wa juu ya sikio.
“Jones ni mjomba wangu, ameuawa kwa kuchinjwa hapa kwenye
koromeo. Amekatwa na panga hapa kichwani na eneo hili la juu ya sikio. Lakini
tumekuta mabegi yamefunguliwa, labda alikuwa akitafuta fedha.
“Binafsi nina shaka huenda mjomba wangu ameuawa kwa
sababu za fitna au fedha aliyouza kiwanja huko Buswelu baada ya kulipwa na jiji
na baadaye akaja kujenga huku Buhongwa,” alisema.
Benjamin alisema fundi ujenzi anayetuhumiwa kutekeleza
mauaji hayo aliitwa na Jones na tangu awasili nyumbani hapo alikuwa akilala
kwenye chumba cha watoto.
Alibainisha kuwa familia hiyo ina watoto tisa na
haijulikani kwanini mtuhumiwa hakuwadhuru wengine nane waliokuwamo kwenye
chumba alichokuwa akilala.
Inadaiwa kuwa mtoto aliyeuawa alikuwa amelala na wenzake
na muuaji aliamua kumpeleka kwa mama yake ili akanyonye na ndipo alipokwenda
kumnyonga.
Musa Sayi, mkazi wa Buhongwa alisema walipata taarifa za
mauaji hayo jana alfajiri na walipofika walihisi kuna mtu amemaliza kuoga
lakini hawakumuona.
“Mazingira tuliyoyakuta pale tulihisi kuna mtu anaoga,
lakini hatukuona. Tulihisi ndiye muuaji labda amefanya mitambiko ya kichawi,”
alisema.
Jeshi la Polisi kupitia kwa Mkuu wa Kitengo cha
Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Mwanza, Joseph Konyo (RCO), alisema Jones
aliuawa kwa kukatwa panga kichwani na upande mmoja wa juu ya sikio, na si kuchinjwa
kama kuku.
“Huyu baba mwenye nyumba yeye ameuawa kwa kukatwa panga
katikati ya kichwa na likaingia sana na huku upande wa karibu na sikio.
Hajachinjwa kama baadhi ya watu wanavyodai,” alisema.
Konyo alisema walifika eneo la tukio hilo na kushuhudia
miili ya marehemu hao.
Akizungumzia tukio la jana, RCO Konyo alisema yawezekana
chanzo cha mauaji hayo yanatokana na fitna, visa na uhasama wa muda mrefu baina
ya mwenye nyumba na baadhi ya watu na kuna uwezekano muuaji hakuwa peke yake.
Kamanda Konyo alisema polisi itawasaka wauaji hao ili
iwafikishe kwenye vyombo vya sheria.
Tukio kama hilo limewahi kutokea Februari 16, 2010 huko
Musoma mkoani Mara, baada ya watu 17 wa familia tatu za koo moja kuuawa kinyama
na wengine watatu kujeruhiwa vibaya pamoja na ng’ombe kadhaa kuchinjwa huko
Buhare.
Mauaji hayo ya Musoma yalielezwa kwamba yalikuwa ya
kulipiza kisasi, baada ya kutokea wizi wa mifugo kisha watu kadhaa kuuawa miaka
ya nyuma kabla ya mwaka huo 2010.
CHANZO: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment