KWA mara ya kwanza tangu kujipatia uhuru wake, Kenya
haitawakilishwa katika Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa. Kwa mujibu wa taarifa
kutoka Ikulu ya Nairobi, Balozi na mwakilishi wa kudumu wa Kenya kwenye Umoja
huo, Machariah Kamau, alimtaarifu katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon
kuwa Kenya haitahudhuria kwenye Hadhara Kuu inayotarajiwa kufanyika hivi
karibuni.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa Rais Kenyatta asingeweza kuwa
nje ya nchi wakati ambao Makamu wake pia hayupo nchini. Makamu wa Rais wa
Kenya, William Ruto yuko nchini Uholanzi akihudhuria vikao vya kesi
inayomkabili kwenye mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC).
Wiki moja kabla ya kuanza kwa kesi ya Ruto, Kenyatta
alikuwa ameonesha kuwa isingewezekana kwa viongozi wote wawili kuwa kuwa nje ya
nchi kwa wakati mmoja. Wakati huo ICC ilikuwa imeshatoa ratiba ya awali
iliyoonesha kuwa wote wawili wangeweza kuwa mahakamani kwa wakati mmoja.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Kenya ilimwambia Katibu Mkuu
wa Umoja wa Mataifa kuwa nafasi ya kisiasa ya kuendelea uhusiano ilikuwa
ikizorota na nchi hiyo ilikuwa ikihofia matokeo mabaya kutokana na mwenendo wa
waendesha mashitaka wa ICC.
Kenyatta alikuwa amepangiwa kuhudhuria Kikao cha Mkutano
Mkuu wa Umaoja wa Mataifa kuanzia Septemba 23 mpaka Septemba 27.
Aidha, Rais Kenyatta amemwita Nairobi Balozi wa Kenya
kwenye Umoja huo, Macharia Kamau, kwa mashauriano.

0 comments:
Post a Comment