RAIS wa mpito nchini Misri, Adly Mansour
ameongeza muda wa hali ya hatari kwa muda wa miezi miwili zaidi kutokana na
hali ya usalama kuendelea kuzorota.
Serikali imesema katika tangazo lililotolewa
na Rais leo kuwa uamuzi huo umefikiwa kutokana na hali ya usalama ilivyo nchini
humo.
Tangazo hilo linakuja siku kadhaa kabla ya
kufikia kikomo kwa muda wa hali ya hatari uliowekwa mwezi Agosti.
Nchi hiyo bado inashuhudia maandamano ya
kila siku yakitaka kurejeshwa madarakani kwa rais aliyeuzuliwa, Muhammad Mursi.
Awali serikali hiyo inayoungwa mkono na
jeshi, ilitangaza hali ya hatari baada ya watu kadhaa kuuawa kufuatia vikosi
vya usalama kuzivunja kambi mbili za waandamanaji waliokuwa wakimuunga mkono
Mursi. Zaidi ya watu 1300, wengi wao wakiwa wafuasi wa Mursi, wameuawa katika ghasia
zinazoendelea.
Serikali ya rais Mansour aliyeteuliwa na
jeshi, ilianzisha operesheni ya kukabiliana na wafuasi wa Mursi na zaidi ya
wanachama 2,000 wa vuguvugu la Udugu wa Kiislamu wametiwa korokoroni, akiwemo kiongozi
mkuu wa vuguvugu hilo, Muhammad Badie.
Mauaji hayo yameamsha lawama za kimataifa na
kuzitaka taasisi huru kufanya uchunguzi juu ya ghasia hizo.
Aidha, siku ya Jumatatu, Kamishina mkuu wa
Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu, Navi Pillay, alitoa wito wa kufanyika
uchunguzi wa mauaji hayo.
"Njia ya kuelekea kwenye uthabiti
nchini Misri inategemea uthabiti wa utawala wa sheria katika hali inayohakikisha
kuwa Wamisri wote, bila kujali mrengo wao wa kisiasa, jinsia, dini au wadhifa,
wanatambuliwa kama wadau halali wa mustkbali wa nchi yao,” alisema.
Mwezi Julai, jeshi lilimuondoa madarakani
Mursi, kusimamisha matumizi ya katiba na kulivunja bunge.

0 comments:
Post a Comment