
WAKAGUZI wa Umoja wa Mataifa wamethibitisha kutumika kwa
silaha za kemikali katika shambulizi moja lililofanyika mwezi uliopita karibu
na mji mkuu wa Syria, Damascus, lakini haikuunyooshea kidole upande wowote.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo iliyotolewa leo na Katibu Mkuu
wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, sampuli za kemikali zilizochukuliwa
zinaonesha kuwa makombora ya ardhini yenye sumu ya sarin yalitumika katika eneo
la Ghouta Agosti 21.
"Tunahitimisha kwamba silaha za kemikali zimetumika
katika mgogoro unaoendelea baina ya pande mbalimbali katika Jamhuri ya Kiarabu
ya Syria…dhidi ya raia, wakiwemo watoto, kwa kiwango kikubwa,” inasema ripoti
hiyo.
Mamia ya watu waliuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa
katika shambulizi moja la kemikali katika viunga vya Damascus vya Ain Tarma,
Zamalka na Jubar mnamo Agosti 21.
Makundi ya upinzani nchini humo yalidai kuwa shambulizi
hilo lilifanywa na jeshi la utawala wa Damascus.
Hata hivyo, serikali imekuwa ikikanusha vikali madai
hayo na kusema kuwa shambulizi hilo lilifanywa na makundi ya waasi ili kuchochea
ghadhabu ya jumuiya ya Kimataifa dhidi ya serikali hiyo na ili kuweka shinikizo
la uingiliaji kijeshi kutoka nje.
Kufuatia shembulizi hilo, Marekani ilitaka kuchukuliwa
kwa hatua ya kijeshi dhidi ya Damascus. Serikali ya Syria iliepusha hujuma hiyo
ya kijeshi kwa kuukubali mpango wa Urusi wa kuyaweka maghala yake ya silaha za
kimataifa chini ya uangalizi wa kimataifa na kisha ziharibiwe.
0 comments:
Post a Comment