Septemba 13, 2013
Kwa mara nyengine tena tukio la kinyama na la aibu
limetokea kwa matumizi ya tindi kali dhidi ya binaadamu ambapo leo hii Kiongozi
wa Kidini akiwa ni Padri Joseph Magamba, alieshambuliwa akiwa maeneo ya
Mkamasini, Mjini Unguja.
Vijana wa Umoja wa Kitaifa Zanzibar (VUK) lina laani
tukio hilo kwa nguvu zote na hakuna sababu yoyote ile ya kutumia tindi kali
kama silaha dhidi ya binaadamu.
VUK inasikitishwa na matendo kama haya ambayo yanazidi
kujenga uadui baina ya Wazanzibari ambapo huu ni wakati wa Wazanzibari kuwa
pamoja zaidi na wazuie vishawishi vyovyote vya kuwagawa.
Kama ambavyo inalaani matumizi kwa binadaamu yoyote pia
inalaani matumizi ya tindi kali dhidi ya viongozi wa kidini na inasimama kuwa
hakuna sababu yoyote ile ya kufanya hivyo ama kwa njia ya kisasi, mgogoro kwa
sababu njia za amani hazijafungwa na kwa hakika zimezoeleka kutumika na
Wazanzibari.
VUK inawataka wananchi kushikamana, lakini hasa vijana
wasikubali kuingizwa katika matukio kama hayo lakini pia wasishabikie na zaidi
wasiwafiche waovu kama hawa kwa kuwatolea ripoti kwa mamlaka za ulinzi na
usalama.
VUK inawataka wananchi kujua matukio kama haya sio tu ya
hatari, lakini pia wanachafua jina na amani ya nchi na kwa hivyo wakati huu
ndio muwafaka kwa kila mwananchi kuwa macho na kuwa mlinzi wa watu ambao
wanataka kuiharibia sifa na jina jina la Zanzibar.
VUK inalitaka Jeshi la Polisi na Idara ya Usalama wa
Taifa itoe majibu ya matukio kama haya ambayo sasa yanachafua akhlaki na
utengamano wa Wazanzibari, na majibu hayo tunayataka leo kabla ya kesho maana
kuanzia kesi ya Sheikh Fadhil Soraga, Sheha wa Tomondo na pia vijana wawili wa
Kiingereza ambao ni Katie Gee (18) na Kirstie Trup (18).
VUK inavitaka vyombo hivyo virudishe imani ya
Wazanzibari ambao wamezoea jamii inayoishi kwa kupendana na kusaidiana na
ambapo sasa inafisidika kwa kuchukina na unyama.
Pia VUK inatoa wito kwa Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar kutumia kila aina ya uwezo iliyonayo, na kwa umma kuona uwezo huo
unatumika, kuhakikisha kuwa wahusika wanakamatwa na kuchukuliwa hatua.
Vilevile SMZ ihakikishe inadhibiti upatikanaji na
usambazaji wa tindi kali, ambayo hivi sasa inaonekana kupatikana kwake ni
rahisi na matumizi yake ni hatari kwa umma.
Kila mtu ajue na aone kuwa anaweza kuwa hatarini
kushambuliwa kwa silaha hii na hivyo wajibu wa kuchukia na kuchukua hatua ni wa
kila mtu lakini hasa vijana ambao wao huwapo mitaani saa zote.
VUK ina mpa pole Padri Joseph Magamba na inamuombea
Mungu ampe afueni ya haraka na tunaungana na jamaa na waumini wake katika
kipindi hiki kigumu
Salum Abdallah Salum
Kaimu Mwenyekiti
0713742255
USULI:
Vijana wa Umoja wa Kitaifa (VUK) ni Vuguvugu la Vijana
wa Kizanzibari linalopenda maendeleo na mabadiliko na ambalo linajumuisha
vijana wa Kizanzibari wa aina mbali mbali bila ya kujali tofauti zao za kidini,
kiitikadi na kimaeneo.

0 comments:
Post a Comment