![]() |
| Rais wa Zambia Michael Sata |
RAIS wa Zambia, Michael Sata ametishia kulivunja bunge
la nchi hiyo akiwatuhumu mawaziri kushindwa kuitetea serikali dhidi ya
mashambulizi ya upinzani.
Habari hiyo imekuja baada ya utawala wa Sata ambao upo
madarakani kwa miaka miwili sasa kushutumiwa kwa kuwa na mawaziri wengi.
"Kwa nini hamzungumzi? Kwa nini mnakaa kimya?”
aliuliza Sata katika kikao chake na baraza la mawaziri leo.
"Kama hamuwezi kuwa mnavyotakiwa kuwa niambieni ili
nilivunje bunge na kuitisha uchaguzi mkuu.”
Vyama vya upunzani nchini humo vimelikosoa vikali baraza
hilo, wakimtuhumu Sata kuwa na mawaziri wengi, ambao ni maswahiba wa rais.
Kwa mujibu wa katiba ya Zambia, uchaguzi mpya unapaswa
kufanyika ndani ya siku 9 iwapo bunge litavunjwa.
Sata aliwataka mawaziri kujibu shutuma kutoka vyama vya
upinzani, hususan kutoka kwa kiongozi wa chama cha United Party for National
Development (UPND), Hakainde Hichilema.
"Tunachafuliwa kushoto, kulia na katikati. Leo Hichilema
anasema baraza hili la mawaziri limevimbiwa, siku nyingine akasema baraza hili
ni la ukoo na nyinyi mnakaa kimya bila kumjibu… mnadhani nani atakayewajibia?”
alisema Sata.
Uchaguzi mkuu wa Zambia umepangwa kufanyika mwaka 2016.

0 comments:
Post a Comment