
Uamuzi wa dhamana ya mshtakiwa Sheikh Ponda Issa Ponda
anayekabiliwa na mashtaka matatu unatarajia kutolewa Septemba 17 (leo) katika
Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Morogoro, baada ya Mahakama hiyo kupitia
vifungu vya sheria kutokana na upande wa utetezi kuwasilisha ombi la dhamana
wakati upande wa mashtaka ukipinga dhamana ya kiongozi huyo.
Ombi la dhamana ya Sheikh Ponda liliwasilishwa
mahakamani hapo Agosti 28 na wakili wake, Juma Nasoro mbele ya Hakimu Mkazi
Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Richard Kabate baada ya wakili huyo kuiomba Mahakama
kumpatia dhamana kiongozi huyo kwa madai kuwa kutokana na mashtaka hayo, mteja
wake kisheria anayo haki ya kupatiwa dhamana.
Pamoja na kuomba mteja wake kupatiwa dhamana, pia Wakili
Nassoro aliwasilisha ombi la kupatiwa hati yenye maelezo ya mlalamikaji wa kesi
hiyo ambaye ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwani alidai kuwa anahitaji
maelezo hayo kwa ajili ya kuandaa utetezi.
Licha ya kuwasilishwa maombi hayo mahakamani hapo,
upande wa mashtaka ukiongozwa na Wakili wa Serikali, Bernad Kongola ulipinga
dhamana ya mshtakiwa huyo kwa madai kuwa ombi hilo halina msingi wowote na
kwamba kutokana na cheti kilichotolewa na Mkurugenzi wa Mashtaka nchini DPP,
kimepinga dhamana ya mshtakiwa huyo kwa maslahi ya usalama wa nchi.
Kutokana na mvutano kati ya pande hizo mbili, Hakimu
Kabate aliahirisha kesi ili aweze kupata nafasi ya kupitia vifungu mbalimbali
vya sheria, ambapo leo atatoa uamuzi wa kumpa ama kutompa dhamana mshtakiwa
huyo ambaye anakabiwa na shtaka la uchochezi, kuharibu imani za dini za watu
wengine na kushawishi kutenda kosa ambayo aliyatenda Agosti 10 mwaka huu eneo
la Kiwanja cha Ndege Manispaa ya Morogoro.
Pamoja na kutoa uamuzi wa dhamana, pia kesi hiyo
itasomwa na kupangiwa tarehe ya kuanza kusikilizwa, kwani upande wa mashtaka
ulidai kuwa umekamilisha upelelezi ambapo wanatarajia kupeleka mashahidi 15 na
vielelezo zikiwamo DVD mbili na kibali cha kongamano la Eid lililoandaliwa na
Umoja wa Wahadhiri Mkoani Morogoro ambalo mshtakiwa anadaiwa kutenda makosa
hayo akiwa katika kongamano hilo.
0 comments:
Post a Comment