Rais Jakaya Kikwete amezungumza kwa simu na rais Uhuru
Kenyatta wa Kenya na kumpa pole na kutaka kujua jinsi gani Tanzania inaweza
kusaidia kufuatia shambulio la kigaidi kwenye kituo cha biashara cha Westgate
katika eneo la Westlands, Nairobi, ambako watu 62 wameuawa na wengine 175
wamejeruhiwa.
Rais Kikwete alimpigia simu rais Kenyatta jioni ya Jumamosi kutokea mjini New York, marekani, mara baada
ya kuwasili mjini humo akitokea Toronto, canada, ambako alifanya ziara ya kikazi
ya siku tatu. Katika mazungumzo kati ya viongozi hao, rais Kikwete amemweleza
rais Kenyatta mshtuko na hasira yake kutokana na taarifa za kusikitisha za
shambulio hilo la kigaidi .
Rais Kikwete amefuatilia mazungumzo hayo kwa salamu
rasmi za rambirambi ambazo rais Kikwete amemtumia rais Kenyatta akielezea
masikitiko na hasira yake kufuatia mauaji hayo ya watu wasiokuwa na hatia
akitaka kujua jinsi Tanzania inaweza kusaidia juhudi za serikali ya Kenya
katika kukabiliana na madhara ya tukio hilo na balaa la ugaidi kwa jumla.
Katika salamu zake rais Kikwete amesema shambulio hili
linalenga kuitisha serikali na wananchi hodari wa Kenya na kudhoofisha nia yao
ya kutimiza wajibu wao wa kihistoria wa kuunga mkono jitihada za kuleta amani
katika nchi jirani na yenye matatizo ya Somalia. Rais amesema kwa maana hiyo,
shambulio hilo la woga na lisilo na huruma kabisa dhidi ya watu wasiokuwa na
hatia, lazima lilaaniwe na kushutumiwa vikali na wapenda amani wote.
Amesema serikali na wananchi wa jamhuri ya muungano wa
Tanzania wanasimama bega kwa bega na kaka na dada zao wa Kenya katika kipindi
hiki kigumu. Aidha, serikali ya Tanzania inapenda kuihakikishia serikali ya
Kenya itaendelea kuiunga mkono na kushirikiana nayo katika kupambana na balaa
la ugaidi katika sura zake zote.
CHANZO: ITV
0 comments:
Post a Comment