MAHAKAMA mjini Cairo imezifungia na kuzipiga marufuku
shughuli zote za vuguvugu la Udugu wa Kiislamu kama taasisi isiyokuwa ya
Kiserikali, kwa mujibu wa duru za kimahakama.
Hukumu ya mahakama hiyo inajumuisha kuzishikilia mali,
rasilimali na makao makuu ya vuguvugu hilo.
"Mahakama inapiga marufuku shughuli za vuguvugu la Udugu
wa Kiislamu na taasisi yake isiyokuwa ya Kiserikali na shunguli zote
inazoshiriki na taasisi yoyote inayotokana nacho,” vyombo vya habari vilimnukuu
jaji Mohammed al-Sayed akisoma hukumu hiyo.
Mahakama imelipa baraza la mawaziri pendekezo la kuunda
kamati huru kufuatilia utekelezaji wa hukumu hiyo.
Wengi wanaamini kuwa hukumu hiyo inaandaa uwanja kwa
jeshi kuwatia nguvuni waandamanaji wanaliunga mkono vuguvugu hilo.
Jumuiya ya Udugu wa Kiislamu ilianzishwa mapema mwaka
huu kama Taasisi isiyokuwa ya Kiserikali (NGO). Kiongozi wa zamani wa vuguvugu
hilo, Mohammed Mahdi Akef, ndiye
aliyekuwa mwenyekiti wake. Viongozi wa jumuiya hiyo si wote wanaotoka katika
vuguvugu hilo au Chama chake cha Uhuru na Uadilifu.
Chama cha Uhuru na Uadilifu ambacho ni tawi la kisiasa
la vuguvugu hilo kilishinda uchaguzi wa bunge na urais baada ya kiongozi wa
zamani wa taifa hilo, Husni Mubarak, kung’olewa katika mapinduzi ya wananchi ya
mwaka 2011.

0 comments:
Post a Comment