PUTIN: TUNA MIKAKATI YETU IWAPO SYRIA ITASHAMBULIWA


Russian President Vladimir Putin



Rais wa Urusi, Vladimir Putin amesema nchi yake ina mipango yake ya kulishughulikia shambulizi linaloweza kutokea dhidi ya Syria.

Putin aliyasema hayo juzi wakati wa mahojiano maalumu aliyoyafanya na shirika la habari la Associated Press na televisheni ya serikali ya Channel 1 yaliyochapishwa jana Jumatano.

"Tuna mawazo yetu kuhusu tutakachokifanya na jinsi tutakavyokifanya iwapo itatokea hali ya matumizi ya nguvu au vinginevyo. Tuna mikakati na mipango yetu, lakini ni mapema mno kuizungumzia,” alisema.

Tishio la kuishambulia Syria liliongezeka baada ya serikali ya Rais Bashar al-Assad kutuhumiwa kwamba ilitumia silaha za sumu kwenye maeneo yanayodhibitiwa na waasi kwenye viunga vya mji wa Damascus mnamo Agosti 21 mwaka huu.

Syria imekuwa ikikanusha vikali tuhuma hizo, ikisema kuwa shambulizi hilo lilitekelezwa na waasi wenyewe ili kuipaka matope.

Mnamo Agosti 31, Rais wa Marekani, Barack Obama, aliiambia dunia kuwa ameamua kwamba Marekani lazima ichukue hatua ya kijeshi dhidi ya serikali ya Damascus bila kusubiri kibali na idhini ya Umoja wa Mataifa.

Obama alisema kuwa licha ya kwamba ameshaamua hivyo, atalipeleka suala hilo kwenye bunge la Congress la nchi hiyo. Lakini aliongeza kuwa amejiandaa kutoa amri ya kuishambulia Syria wakati wowote.

Aidha, kwa mara nyingine, Obama aliibebesha serikali ya Damascus lawama za kuhusika na shambulizi la silaha za sumu lililotokea jirani na mji wa Damascus.

Mnamo Agosti 29, kikao cha wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kilimalizika bila kufikia muafaka kuhusu Syria.

Wanachama wa baraza hilo kutoka upande wa Magharibi wamekuwa wakishinikiza kupitishwa azimio la kutumia nguvu za kijeshi, lakini Urusi na China zimekuwa zikipinga vikali mno.

Tangu Machi 2011, Urusi na China zimeshatumia kura ya turufu dhidi ya maazimio matatu ya Baraza hilo yaliyopendekezwa na mataifa ya Ulaya yakitishia kuchukua hatua za kijeshi na vikwazo mbalimbali dhidi ya Damascus.

Aidha, nchi hizo mbili zinapinga shinikizo la sasa kutoka Marekani na Ufaransa la kutaka kuishambulia kijeshi Syria, na zimeapa kutumia kura ya veto dhidi ya azimio lolote linalohalalisha hatua ya kijeshi dhidi ya Damascus.


Share on Google Plus

About mahamoud

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment