· Ni muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Mabadiliko ya Katiba
· Wabunge wa Chadema,Cuf,NCCR-Mageuzi watoka bungeni
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Mabadiliko ya Katiba wa Mwaka 2013 umeligawa Bunge, baada ya wabunge kutoka vyama vya Chadema, NCCR-Mageuzi na CUF kususia mjadala wa muswada huo na kutoka nje ya ukumbi wa Bunge na kuwaacha wabunge wa CCM na Augustine Mrema wa TLP.
Tukio hilo lilitokea katika kikao cha jioni na kusababisha baadhi ya viti vya ukumbi huo kubaki vitupu.
Wabunge waliotoka walikuwa wakitaka mjadala huo usitishwe wakidai hadi hapo wadau kutoka visiwani Zanzibar watakaposhirikishwa kuutolea maoni muswada huo kabla ya kuwasilishwa bungeni.
Wabunge hao walitoka nje muda mfupi baada ya Mbunge wa Viti Maalum (CCM), ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala, Pindi Chana, kuanza kuchangia mjadala huo.
Muswada huo uliwasilishwa bungeni jana na Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe na baadaye Mbunge wa Karagwe (CCM), Gosbert Blandes, aliwasilisha maoni ya Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala na kufuatiwa na Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni wa Wizara ya Katiba na Sheria, Tundu Lissu, kuwasilisha maoni ya kambi hiyo kuhusu muswada huo.
Kitendo cha wabunge hao kususia mjadala huo na kutoka nje ya ukumbi wa Bunge, huku wakitoa sauti za kuzomea kilimfanya Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai, kushikwa na butwaa kwa dakika kadhaa, kabla ya kuhamaki na kuanza kuwataka wabunge hao kutoka vizuri.
“(Wabunge) Mnaotoka, mtoke vizuri, nawaona na mnanifahamu vizuri,” alisema Ndugai, ambaye alisistiza kwamba, mambo yote yaliyolalamikiwa na wabunge yatapelekwa kwenye kamati zinazohusika, ikiwamo ya Kanuni na Uongozi wa Bunge na kisha kuruhusu mjadala, ambao uliendelea.
MNYAA AOMBA MWONGOZO
Kabla ya wabunge hao kuchukua hatua hiyo, Mbunge wa Mkanyageni (CUF), Mohammed Habib Mnyaa, aliomba Mwongozo wa Spika, akihoji uhalali wa Bunge kuendelea na mjadala kuhusu muswada huo, wakati upande wa Zanzibar hawakupewa fursa ya kuutolea maoni.
Baada ya Mnyaa kuomba Mwongozo huo, Ndugai alisimama na kusema atautolea majibu baadaye na kuamuru mjadala kuhusu muswada huo uendelee.
Hoja kuhusu Wazanzibari kutopewa fursa ya kuutolea maoni muswada huo, ilitolewa na Lissu, wakati akiwasilisha maoni ya kambi hiyo bungeni jana.
Lissu, ambaye ni Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema) na Mnadhimu Mkuu wa Kambi hiyo, alisema katika kutekeleza majukumu yake ya kuuchambua muswada huo, Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala ilikutana na wadau wengi mbali mbali.
Alisema katika kukutana na wadau hao, ilipata maoni ya taasisi za kidini na za kiraia; taasisi za elimu ya juu na za kitaaluma; vyama vya siasa na asasi nyingine.
Hata hivyo, alisema kwa sababu, ambazo kamati haikuelezwa vizuri na uongozi wa Bunge, mapendekezo ya kamati kwenda Zanzibar kwa lengo la kukusanya maoni ya wadau wa Zanzibar juu ya muswada huo yalikataliwa.
“Kwa maana hiyo, ni muhimu Bunge lako tukufu lifahamu ukweli huu kwamba wadau pekee walioshirikishwa kutoa maoni yao juu ya muswada ni Watanzania Bara tu. Wazanzibari hawakupatiwa fursa hiyo na hawakushirikishwa kabisa, licha ya Sheria yenyewe kuwa na mambo mengi yanayoihusu Zanzibar,” alisema Lissu.
Kutokana na hali hiyo, alisema Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka kujua sababu za uongozi wa Bunge na wa serikali kuona siyo busara na sahihi kuwapatia Wazanzibari fursa ya kutoa maoni yao kuhusu nuswada huo wa kurekebisha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ambayo inawahusu pia Wazanzibari na nchi yao.
Hata hivyo, Chana alitoa taarifa na kuliambia Bunge kuwa kamati yake ilikwenda Zanzibar na kualika wajumbe mbalimbali, wakiwamo Wazanzibari, Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Chama cha Wanasheria wa Zanzibar pamoja na maofisa wa ZEC, ambao alisema wote walitoa maoni yao mbele ya kamati hiyo.
“Bunge haliwezi kutumika kutimiza matakwa binafsi ya watu mbalimbali,” alisema Chana.
Baadaye, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, alisimama na kuomba kutoa taarifa, na kuliambia Bunge kwamba, makundi yote muhimu, vikiwamo vyama siasa na hata Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, walishirikishwa.
Alisema yeye pamoja na Mwanasheria Mkuu awa Serikali (AG), walikwenda Zanzibar kwa kazi hiyo na kwamba, wameliachia Baraza la Wawakilishi la Zanzibar kupeleka maoni.
KAULI YA CHIKAWE
Awali, Waziri Chikawe alisema muswada huo unapendekeza mambo mbalimbali, ikiwamo kuzuia mahakama kuhoji maoni yatakayotolewa na wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba.
Alisema muswada huo unapendekeza pia Rasimu ya Katiba ijadiliwe kwa siku zisizozidi 70 tangu kuwasilishwa katika Bunge hilo.
Naye Blandes akiwasilisha maoni ya Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala, alisema kamati ilikubaliana na hoja kuhusu Rais kubaki na mamlaka ya kuteua wajumbe wa Bunge hilo kwa kuzingatia makundi mbalimbali ya kijamii.
Alisema kamati pia inakubaliana na idadi ya wajumbe wa Bunge hilo ibaki watu 166 kama inavyopendekezwa na muswada huo.
Wakati tunakwenda mitamboni, wabunge wa vyama vya Chadema, CUF na NCCR Mageuzi walikuwa wamejifungia katika ukumbi wa Pius Msekwa wakijadili.
Hata hivyo, habari kutoka ndani ya kikao hicho zinasema kuwa msimamo wao ni kwamba leo wataingia bungeni katika kipindi cha maswali na majibu na mjadala wa muswada huo utakapoanza watasusia tena.
Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, alisema taarifa rasmi zitatolewa leo.
BUNGE KUAHIRISHWA KESHO
Wakati huo huo, Mkutano wa 12 wa Bunge unatarajiwa kuhitimishwa kesho badala ya Septemba 13 kama ratiba ya awali ilivyoonyesha.
Mwenyekiti wa Bunge, Jenister Mhagama, aliyasema hayo jana muda mfupi baada ya kipindi cha Maswali bungeni kumalizika akisema kuwa hatua hiyo inatokana na serikali kuamua kuiondoa bungeni miswada mitatu ya sheria iliyokuwa imepangwa kujadiliwa.
Alisema miswada ya sheria iliyoondolewa ni pamoja na Muswada wa Sheria ya Takwimu wa mwaka 2013, Muswada wa Sheria wa Kura ya Maoni wa mwaka 2013 na Muswada wa Sheria wa Mfuko wa Wastaafu wa GEPF wa mwaka 2013.
Kuondolewa kwa miswada hiyo kunafanya ibaki miswada mitatu ya kuwasilishwa bungeni ikiwamo wa Sheria ya Taifa wa Umwagiliaji na Muswada wa Sheria wa Vyama vya Ushirika ambayo tayari imejadiliwa na wabunge na kupitishwa.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Mabadiliko ya Katiba wa 2013 utahitimishwa kesho.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:
Post a Comment