Aliyekuwa Rais wa Misri, Muhammad Mursi, ameapa
kupambana mpaka pumzi yake ya mwisho dhidi ya mapinduzi ya kijeshi
yaliyomuondosha madarakani mwezi Julai mwaka huu.
Mapema jana, mmoja wa mawakili wa Mursi, bwana Mustafa
Atteyah, alisema kuwa kiongozi huyo alifanya mazungumzo ya simu na familia yake
kwa mara ya kwanza tangu jeshi lilipomuweka kizuizini.
Shirika la habari la Uturuki la Anadolu, lilikinukuu
chanzo kilicho karibu na familia ya Mursi kikisema kuwa wakati wa mazungumzo
hayo, Mursi aliiambia familia yake kuwa “ataendelea na msimamo wake mpaka pumzi
ya mwisho”.
Kwa mujibu wa chanzo hicho, Mursi bado anajihesabu kuwa “rais
halali” wa taifa hilo la kaskazini mwa Afrika.
Mazungumzo ya Mursi na familia yake yanakuja baada ya
televisheni ya serikali kutangaza Septemba 14 kuwa kiongozi huyo aliyeuzuliwa
atafikishwa mahakamani kujibu mashitaka ya “kuhamasisha mauaji na ghasia” zilizotokea
mwezi Desemba 2012, baada ya pande mbili hasimu zilipopambana mjini Cairo.
Mgogoro ulishtadi nchini Misri tangu Julai 3 baada ya
jeshi la nchi hiyo kumuondosha Mursi madarakani. Vilevile jeshi lilisitisha
matumizi ya katiba na kulivunja bunge.
Mamia ya waandamanaji, wengi wao wakiwa wafuasi wa
Mursi, waliuawa na kujeruhiwa katika ghasia mbaya zilizoikumba nchi hiyo
kufuatia hatua hiyo ya jeshi.
Vikosi vya usalama vimeanzisha operesheni maalumu dhidi
ya chama cha Mursi. Zaidi ya wafuasi 2,000 wa chama hicho wametiwa nguvuni
tangu kuondolewa kwa Mursi, akiwemo kiongozi mkuu wa chama hicho, Muhammad
Badie.
0 comments:
Post a Comment