WAASI nchini Syria wanasema kuwa wanahisi kuwa
wameangushwa na Rais Barack Obama kutokana na uamuzi wake wa kulizingatia
pendekezo la Urusi linalokusudia kuutafuta suluhu ya kidiplomasia mgogoro wa
nchi hiyo uliodumu kwa miaka miwili na nusu.
Jana Jumatano, wapiganaji kadhaa walielezea ghadhabu yao
kutokana na uamuzi wa Washington kusimamisha kwa muda suala la vita na kuipa
nafasi demokrasia.
"Watu walikuwa wana matumaini kuwa Marekani
itafanya mashambulizi yatakayoleta suluhisho, lakini tulitarajia kuwa hakuna
mbacho kingetokea kwa sababu hakuna mwenye suluhu kwa mgogogro wa Syria,”
walisema wapiganaji hao.
Siku moja kabla, Muungano wa Baraza la Kitaifa la Syria
(SNC) ulisema katika taarifa yake kuwa Marekani inapaswa kuendelea na mpango
wake wa kuishambulia Syria ili kuwapa waasi hao nafasi ya kushinda vita dhidi
ya serikali ya Rais Bashar al-Assad.
Shinikizo la kuishambulia Syria liliongezeka baada ya
serikali ya Assad kuhuhumiwa kuwa ilitumia silaha za kemikali kwenye viunga vya
mji wa Damascus tarehe 21 Agosti.
Hata hivyo, serikali ya Damascus imekanusha vikali madai
hayo na kusema kuwa waasi ndio waliotumia silaha hizo za sumu ili kuamsha moto
wa hasira dhidi ya utawala wa Bashar.
Juzi Jumanne, Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria, Walid
al-Muallem, alisema kuwa serikali ya Damascus iko tayari kutekeleza pendekezo
lililotolewa na Urusi la kuyaweka maghala ya silaha za kemikali chini ya
udhibiti wa Umoja wa Mataifa.
Serikali ya Urusi ilitoa pendekezo hilo wakati wa
mkutano baina ya Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Urusi, Sergei Lavrov na waziri
Muallem mjini Moscow Jumatatu iliyopita.
"Tunataka kuingia katika mkataba wa kupiga marufuku
silaha za kemikali. Tuko tayari kutekeleza wajibu wetu kulingana na mkataba
huo, ikiwemo kutoa taarifa zote kuhusu silaha hizi,” alisema Muallem.
Katika kujibu hatua hiyo, Rais wa Marekani aliliomba
bunge la Congress la nchi yake kuakhirisha zoezi la upigaji kura ya kuidhinisha
vita dhidi ya Syria ili kulipa nafasi pendekezo la Urusi.
Syria imekuwa katika machafuko makubwa tangu Machi 2011
na zaidi ya watu 100,000 wameshapoteza maisha yao.

0 comments:
Post a Comment