
Waasi wa M23 kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, wameonya kuwa watarudi vitani iwapo serikali ya nchi hiyo itakataa kusitisha mashambulizi yake ya kijeshi na kurudi kwenye meza ya mazungumzo.
Siku ya Ijumaa, jeshi la serikali lilividhibiti vilima muhimu vilivyopo juu ya mji wa Goma baada ya wapiganaji wa M23 kuondoka eneo hilo.
Siku ya Jumamosi, waasi hao ambao walijondoa katika jeshi la serikali mwezi Aprili 2012, walitoa taarifa wakisema kuwa uamuzi wao wa kusitisha mapigano na kuondoka kwenye medani ya mapambano ulilenga “kutengeneza mazingira mazuri” ya kupatikana kwa “suluhisho la kisiasa la mgogoro huo”.
"Tunaitaka serikali ya Kongo irejee haraka kwenye meza ya mazungumzo ili kutafuta suluhu ya kisiasa ya mgogoro huu,” alisema Bisimwa, ambaye ni rais wa kundi hilo.
"Serikali ya Kongo ikiendelea na hatua ya kijeshi badala ya kwenda Kampala kwa ajili ya mazungumzo, vikosi vyetu vitakuwa na haki ya kurejesha udhibiti” wa maeneo ya nje ya mji wa Goma.
Naye msemaji wa jeshi la Kongo, Luteni Kanali Olivier Hamuli alisema kuwa “hawakuondoka kwa hiari, walikutana na nguvu ya jeshi.”
Jeshi la Kongo likisaidiwa na kikosi kipya cha Umoja wa Mataifa chenye jukumu la kupambana, limekuwa likipambana na waasi wa M23 karibu na mji wa Goma kwa siku kadhaa kwa lengo la kuwarudisha nyuma.
Brigedi hiyo ya Umoja wa Mataifa inayoongozwa na Mtanzania, imepewa mamlaka na Baraza la Usalama la Umoja wa Matifa ya kuendesha operesheni za mashambulizi dhidi ya makundi yenye silaha mashariki mwa Kongo.
Novemba 20, 2012, waasi wa M23 waliudhibiti mji wa Goma, baada ya walinda amani wa Umoja wa Mataifa kushindwa kuwazuia kuingia katika mji huo. Waliondoka mjini humo Desemba 1, 2012 baada ya kufikiwa kwa makubaliano ya kusitisha mapigano.
Katika mkutano wa kimataifa uliofanyika Novemba 24 kuhusu Eneo la Maziwa Makuu, serikali ya Kongo iliahidi kuanzisha mazungumzo ya amani na waasi wa M23.
Mazungumzo baina ya serikali ya Kinshasa na waasi wa M23 yalianza Desemba 2012 lakini yakavunjika mwezi Aprili 2013.
Makundi kadhaa yenye silaha, ikiwemo M23, wanaendesha harakati zao za uasi mashariki mwa Kongo na wanapigania kuidhibiti nchi hiyo kubwa yenye maliasili za madini, kama vile dhahabu, urani, coltan, ambayo hutumika katika utengenezaji wa vifaa vingi vya elektroniki, ikiwemo simu za mkononi.
Tangu mwezi Mei 2012, takriban watu milioni 3 wameyekimbia makazi yao katika eneo la mashariki mwa Kongo. Takriban watu milioni 2.5 ni wakimbizi wa ndani, huku zaidi ya watu 460,000 wamekimbilia katika nchi za Rwanda na Uganda.
0 comments:
Post a Comment