OBAMA: MAREKANI IMEAMUA KUISHAMBULIA SYRIA


US President Barack Obama delivering a speech on Syria at the White House, August, 31, 2013


Rais wa Marekani, Barack Obama, amesema kuwa ameamua kwamba Marekani itaishambulia kijeshi Syria baada ya duru za kiintelejensia kudai kuwa Damascus ilitumia silaha za kemikali dhidi ya waasi.

Hata hivyo, alisema kuwa ataomba idhini ya bunge la Congress pindi bunge hilo litakapofunguliwa Septemba 9.

"Kwa siku kadhaa sasa, tumewasikia Wabunge wakitaka sauti zao kusikika,” alisema Obama wakati akizungumza na wanahabari katika ikulu ya White House.

Alisema kuwa viongozi wa Bunge wamekubali kufanya madahalo maalumu kuhusu Syria na kupiga kura pindi watakaporejea Bungeni.

Hata hivyo, Obama hakusema iwapo atatumia mamlaka yake kama amiri jeshi mkuu kuishambulia Syria iwapo Bunge litapinga wito wake huo.

"Wakati nikiamini kuwa nina mamlaka ya kutekeleza shambulizi hili bila idhini maalumu ya Bunge, ninajua kwamba nchi itakuwa imara zaidi iwapo tutatumia utaratibu huu na hatua zetu zitakuwa na nguvu zaidi,” alisema.

Kiongozi wa wajumbe wachache katika bunge la Seneti, Mitch McConnell, aliukaribisha uamuzi huo wa rais.

"Nafasi ya rais kama amiri jeshi mkuu daima hupata nguvu pale anapopata uungwaji mkono wa wazi kutoka Bungeni,” alisema McConnell.


Jana Ijumaa, Marekani ilitoa ripoti ya kiintelejensia ikiituhumu serikali ya rais  Bashar al-Assad ilitumia silaha za sumu kwenye ngome za waasi katika viunga vya mji wa Damascus wiki iliyopita iliyowaua watu 1,429.

Siku za nyuma Obama aliwahi kusema kuwa matumizi ya silaha za kemikali ni “msitari mwekundu” ambao serikali ya Syria haipaswi kuuvuka na iwapo itafanya hivyo itasababisha kuchukuliwa hatua ya kijeshi kutoka Marekani.

Wakati wananchi wa Marekani na baadhi ya Wabunge wakipinga hatua hiyo, Obama alikariri kwamba uingiliaji kati wa kijeshi utakaofanywa na Marekani utakuwa wa “muda mfupi na kiwango kidogo.”

"Halitakuwa shambulizi la kudumu. Hatutakanyaga miguu yetu ardhini,” alisema rais Obama.

Uwezekano wa kutokea kwa mashambulizi uliongezeka baada ya wakaguzi wa Umoja wa Mataifa kuondoka Syria leo Jumamosi, siku moja baada ya Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani, John Kerry, kusema kuwa ushahidi wa serikali ya Assad kutumia silaha za sumu uko “wazi na thabiti.”


Wataalamu hao wa Umoja wa Mataifa walichukua sampulu za damu na mkojo kutoka kwa waathirika na sampuli za udongo kutoka kwenye maeneo yanayodaiwa kuwa silaha za sumu zilitumika. Sampuli hizo zitafanyiwa uchunguzi huko Ulaya. 
Share on Google Plus

About mahamoud

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment