![]() |
| Askari wa jeshi la Kenya (KDF) wakiwasili kwenye kituo cha biashara cha Westgate leo. |
IDADI ya vifo kutokana na shambulizi lililofanywa na
wanamgambo wa Kisomali kwenye kituo kimoja cha biashara mjini Nairobi
imeongezeka na kufikia watu 59 huku idadi rasmi ya wale wanaoendelea
kushikiliwa mateka ikiwa haijulikani.
Leo Waziri wa Mambo ya Ndani wa Kenya, Joseph Ole Lenku alisema:
“Bado kuna watu wanaoshikiliwa mateka ndani ya maduka haya, na hili linafanya
kazi hii kuwa ngumu. Mpaka sasa kuna watu 59 waliouawa.”
Vile vile, Lenku alithibitisha kuwa kwa uchache watu 175
walijeruhiwa katika shambulizi hilo lililoanza jana majira ya saa 5 asubuhi kwa
saa za Afrika Mashariki.
Lenku aliongeza kuwa takriban watu 1,000 wameshaokolewa,
lakini bado kuna idadi ya mateka ambao wanashikiliwa na watekaji ndani ya kituo
hicho cha Westgate.
“Kuna washambuliaji kadhaa ambao bado wapo katika jengo,
na idadi yao inakadiriwa kuwa kumi mpaka kumi na tano,” alisema waziri huyo.
“Tunaamini kuna watu ambao bado wapo ndani ya jengo
hilo, ndiyo maana operesheni hii inakuwa ngumu.”
Polisi pamoja na vikosi vya jeshi la Kenya vinaendesha
operesheni maalumu kumaliza mzingiro huo.
Msemaji mmoja wa kundi la al-Shabab alisema katika
taarifa iliyotolewa jana usiku kuwa kundi lake ndilo lililohusika na shambulizi
hilo.
Mapema jana Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta, aliahidi “kuwasaka
washambuliaji hao kokote watakapokimbilia.”
Mwaka 2011 Kenya ilituma askari 4,000 kusini mwa Somalia
kwenda kuisaidia serikali ya nchi hiyo katika mapambano yake dhidi ya
wapiganaji wa al-Shabaab.
Askari hao wa Kenya ni sehemu ya Kikosi cha Umoja wa
Afrika nchini Somalia (AMISOM) kinachopata mafunzo na zana kutoka nchi wahisani
kwa lengo la kurejesha usalama nchini humo.v

0 comments:
Post a Comment