Ni hivi karibuni tulishuhudia mataifa makubwa
yakilumbana juu ya hatua inayotakiwa kuchukuliwa katika kuutia adabu utawala wa
Rais Bashar al-Assad. Upande mmoja ulikuwa na nchi za Urusi, China, Iran na
waitifaki wao. Huku upande wa pili ukiongozwa na Marekani, Uingereza, Ufaransa
na waitifaki wao.
Upande wa Marekani ulikuwa ukishadidia kuchukuliwa hatua
kali dhidi ya Damascus kwa hoja kwamba utawala wa Assad ulivuka “msitari
mwekundu” kwa kutumia silaha za kemikali kuwaua raia katika shambulizi
lililotokea katika viunga vya mji wa Damascus mnamo Agosti 21.
Baada ya shambulizi, tulimuona Rais Obama akiutangazia
ulimwengu kuwa lazima Assad atiwe adamu kwa kushambuliwa kijeshi, na tukaona
azma hiyo ikiwekwa vitendoni kwa kutuma manowari kadhaa katika bahari ya
Mediterrania.
Kwa upande wa pili alikuwepo Urusi, China na Iran ambao
walishikilia msimamo kuwa silaha hizo zilitumiwa na waaasi katika kutaka
uungwaji mkono wa kimataifa na kutoa onyo kwa Marekani na waitifaki wake
wasijaribu kuishambulia Syria nje ya kanuni za Umoja wa Mataifa.
Na ingawa moto umepoa baada ya muafaka uliofikiwa baina
ya Urusi na Marekani wa kuziweka ghala za silaha za kemikali zinazomilikiwa na
Syria chini ya udhibiti wa kimataifa na kisha kuziteketeza;
Na ingawa Assad alikubaliana na pendekezo hilo na hivyo
kuepusha vita ambavyo vilitazamwa na baadhi ya wachambuzi wa mambo kama ujio wa
“vita ya tatu ya dunia”, na ambavyo
vingeyagharimu maisha ya raia wasiokuwa na hatia; leo nimependa tujikumbushe
kile kilichoachwa na Marekani katika mji mmoja wa Iraq baada ya kuivamia nchi
hiyo kwa kisingizio cha kuzisaka silaha za nyuklia, zilizodaiwa kumilikiwa na
rais wa wakati huo, marehemu Saddam Hussein. Mji huo ni Fallujah, mji
unaopatikana umbali wa maili 30 magharibi mwa Baghdad. Lengo langu ni kujaribu
kudodosa zile athari zinatokana na vita kama hivi kwenye miji mbalimbali
duniani, na hususan Mashariki ya Kati.
Utafiti mpya uliotolewa hivi karibuni umebaini kuwa
ongezeko la vifo vya watoto wachanga, saratani ya damu na matatizo mengine ya
kiafya katika mji wa Fallujah nchini Iraq, ambao ulipigwa mabomu na Marekani
mwaka 2004, ni zaidi ya kile kilichoripotiwa na manusura wa mabomu ya atomiki
yaliyodondoshwa katika miji ya Hiroshima na Nagasaki nchini Japan mwaka 1945.
Madaktari wa Iraq mjini Fallujah wanalalamika kuwa tangu
mwaka 2005 wameendelea kuhemewa na idadi ya watoto wanaozaliwa wakiwa na kasoro
mbalimbali, kuanzia mtoto wa kike aliyezaliwa akiwa na vichwa viwili mpaka wale
wanaozaliwa wakiwa wamepooza miguu na mikono. Pia wanasema kuwa walianza
kushuhudia ongezeko la kutisha la watu wengi wenye saratani kuliko ilivyokuwa
kabla ya vita ya Fallujah iliyopigwanwa baina ya vikosi vya Marekani na wapiganaji
wa Kiiraq.
Madai ya madaktari hao yameungwa mkono na utafiti
unaoonesha ongezeko la mara nne katika saratani zote na ongezeko la mara 12 kwa
saratani ya watoto walio chini ya umri wa miaka 14. Vifo vya watoto wachanga
katika mji huo viko juu mara nne zaidi ya ilivyo katika nchi jirani ya Jordan
na mara nane zaidi ya Kuwait.
Dk. Chris Busby, ambaye ni profesa katika Chuo Kikuu cha
Ulster na ambaye ni miongoni mwa waendeshaji wa utafiti huo uliowahusiha watu 4,800
mjini Fallujah, anasema kuwa ni vigumu kukificha chanzo halisi cha matatizo ya
saratani na watoto wanaozaliwa wakiwa na upungufu katika viungo vyao. Anasema
kuwa “ ili kuwa na athari kubwa kama hii lazima kiwango kikubwa sana cha
kemikali kilitumika mwaka 2004 yalipoanza mashambulizi hayo.”
Meli za kivita za Marekani zilianza kuuzingira na
kuutwanga kwa mabomu ambao upo maili 30 magharibi mwa Baghdad, mwezi Aprili
2004 baada ya wafanyakazi wanne wa kampuni ya ulinzi ya Kimarekani ya Black
Water kuuliwa na miili yao kuchomwa moto. Baada ya miezi 8 ya kuwa mbali na
mji, mwezi Nivemba mji huo ulivamiwa kwa kutumia vifaru na makombora ya angani
yakatumika kuyalenga maeno ya waasi. Baadaye vikosi vya Marekani vilikiri
kwamba vilitumia fosforasi nyeupe na sumu nyinginezo.
Katika mashambulizi hayo, makamanda wa Marekani, kwa
kiasi kikubwa, waliifanya Fallujah kama eneo huru kutumia risasi ili kupunguza
kiwango cha hasara na madhara kwa askari wao. Maafisa wa Kiingereza
walishtushwa mno na hali ya kutozingatiwa madhara na hasara dhidi ya raia wa
Fallujah. Kamanda mmoja wa Kiingereza, aliyekuwa akifanya kazi na vikosi vya
Marekani mjini Baghdad, Brigedia Nigel Aylwin-Foster, anasema: “Wakati wa
operesheni za awali Novemba 2004 mjini Fallujah, usiku mmoja mizinga 40
ilivurumishwa katika eneo dogo la mji huo.”
Kamanda huyo aliongeza kusema kuwa kamanda wa Kimarekani
aliyeamuru matumizi hayo makubwa ya mashambulizi hakuona kuwa kuna umuhimu wa
kuyatolea maelezo kwenye ripoti yake ya kila siku kwa mkuu wa majeshi wa
Marekani. Dk Busby anasema kuwa ingawa hawezi kuanisha aina ya silaha
zilizotumiwa na meli hizo, kiwango cha athari ya kijenitiki kilichowakumba
wakazi wa mji huo kinaonesha kuwa katika maeneo kadhaa urani (uranium)
ilitumika. Anasema: “Ninahisi kuwa walitumia silaha mpya kuyapiga majengo ili
waweze kuzivunja kuta na kuwaua wale waliokuwa ndani ya kuta hizo.”
Uchunguzi huo ulifanywa na timu ya watafiti 11 mwezi
Januari na Februari mwaka huu ambao walizitembelea nyumba 711 za mji wa
Fallujah. Kwa kweli hali inatisha sana.
Uchunguzi huo ulibaini kuwepo kwa ongezeko la matatizo
ya saratani na kasoro katika viungo vya watoto wanaozaliwa. Ilibainika kuwa
vifo vya watoto wachanga ni 80 katika vizazi 1,000 ikilinganishwa na vifo 19
vya nchini Misri, 17 nchini Jordan na 9.7 nchini Kuwait. Ripoti inasema kuwa
aina ya saratani hiyo ni “sawa na ile iliyopatikana kwa manusura wa shambulizi
la mji wa Hiroshima nchini Japan, ambao waliathiriwa na mionzi yenye sumu
kutoka kwenye bomu urani uliogunduliwa katika mabaki ya nyuklia.”
Watafiti waligundua kuwepo kwa ongezeko la mara 38 la
kansa ya damu, mara 10 katika kansa ya matiti na ongezeko kubwa katika matatizo
ya tezi na uvimbe wa ubongo. Hii ni tofauti na manusura wa Hiroshima ambao
walikuwa na ongezeko la mara 17 katika kansa ya damu, lakini mjini Fallujah,
wachunguzi hao wanasema kuwa tatizo sio tu kushamiri kwa kansa bali pia kasi
kubwa ya ugonjwa huo unavyowaandama watu.
Katika utafiti huo kuna jambo la kushangaza. Utafiti
ulibaini kuwa uwiano baina ya watoto wa kiume na wa kike wanaozaliwa
umebadilika. Kabla ya mashambulizi hayo, uwiano ulikuwa watoto wa kiume 1,050
kwa watoto wa kike 1,000, lakini kwa wale waliozaliwa kuanzia mwaka 2005 vizazi
vya watoto wa kiume vilishuka kwa asilimia 18, yaani uwiano ukawa watoto wa
kiume 850 kwa watoto wa kike 1,000. Uwiano wa jinsia ni dalili ya kuwepo kwa
athari ya kijenitiki inayowakumba wavulana zaidi ya wasichana. Mabadiliko kama
hayo katika uwiano wa kijinsia yaligunduliwa pia baada ya tukio la Hiroshima.
Marekani iliamua kucha kutumia mashambulizi mazito
nchini Iraq kuanzia mwaka 2007 kutokana na ghadhabu ya wananchi kutokana na
vitendo vya jeshi lake. Lakini pia kulikuwa na anguko katika huduma za afya na
usafi, kutokana na mashambulizi hayo. Athari ya vita iliyowakumba wakazi wa mji
wa Fallujah ilikuwa kubwa na mbaya kuliko mji mwingine wowote nchini Iraq kwa
sababu, baada ya mwaka 2004, mji huo uliendelea kuzingirwa na kutengwa na miji
mingine ya nchi hiyo. Taathira za vita zilianza kurekebishwa taratibu sana.
Hata hivyo wakazi wa mji huo walikuwa wakiogopa kwenda hospitalini mjini
Baghdad kwa sababu ya vizuizi vingi vya kijeshi katika barabara iendayo katika
mji mkuu huo wa Iraq.
Ikiwa huu ni mji mmoja tu wa Fallujah, vipi kuhusu miji
mingine iliyokumbwa na zahma kama hizi?
Tafakari…

0 comments:
Post a Comment