
Wakati Serikali ikiahidi kuongeza nguvu katika vita
dhidi ya wauza dawa za kulevya nchini, imebainika kuwa kuna mtandao wa
wafanyabiashara wa pombe haramu ya gongo unaopika na kuichanganya na dawa za
mifugo ili kuiongezea ukali.
Mtandao huo unaomiliki mitambo ya kupika gongo katika
eneo la Mto Kizinga uliopo Dambweni, Kata ya Kilungule, wilayani Temeke,
unadaiwa kuchanganya pombe hiyo na dawa ya mifugo aina ya Multivitamin ambayo
hutumika kurutubisha wanyama.
Hata hivyo, uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini
kuwa dawa hiyo huchanganywa na dawa nyingine ambayo haikufahamika mara moja,
kisha kuiweka kwenye gongo ili kuiongezea ukali zaidi.
Wafanyabiashara hao wamekuwa wakipika gongo hiyo katika
eneo hilo kwa miaka zaidi ya 10, huku baadhi ya viongozi wa serikali ya mtaa
wakitajwa kuwalinda.
Kwa mujibu wa uchunguzi, eneo hilo lina mitambo zaidi ya
minne ya kutengeneza gongo na kila mtambo unazalisha pipa moja lenye ujazo wa
lita 200.
Uchunguzi ulibaini kuwa kila siku wanazalisha zaidi ya
lita 800 za gongo ambayo huuzwa kwa rejareja na jumla. Bei ya rejareja kipimo
kinaanzia Sh500 hadi Sh5,000, ambapo bei ya jumla ni Sh38,000 kwa ndoo yenye
ujazo wa lita 20.
Kwa mtu anayefika kwa mara ya kwanza eneo hilo atakutana
na makundi ya watu wakiwa chini ya miti wakijipumzisha wakati wakisubiri pombe
hiyo kuwa tayari, huku wakazi wengine wa eneo hilo wakionekana kuendelea na
shughuli zao kwenye bustani za mboga za majani zilizolimwa kando kando ya mto.
Mbali ya kuwa wanalindwa na baadhi ya viongozi wa mtaa,
wameweka ulinzi wao wenyewe, kwa kuweka vijana zaidi ya 10 ambao hukaa katika
eneo hilo kuhakikisha kuwa mtu anayefika katika eneo hilo wanamtambua.
Ukifika katika eneo ilipo mitambo yao, watu wanaofanya
kazi ya kupika ni wacheshi, wanaojaribu kumsalimia kila mpita njia bila ya kuwa
na hofu yoyote, huku mmojawao ambaye jina lake halikufahamika mara moja akisema
kuwa wao ndio waliotengeneza barabara ya kupita magari inayoingia sehemu hiyo.
Mkazi mmoja wa eneo hilo ambaye hakutaka jina lake
liandikwe gazetini kwa kuhofia usalama wake, alisema watu hao ndiyo wasambazaji
wakubwa wa gongo jijini Dar es Salaam.
“Biashara hii inalipiwa ‘kodi’ kila mwezi, hawa jamaa
huchangishana fedha halafu huwapelekea baadhi ya askari ambao huwalinda
wasikamatwe, kuna wakati huchanga hadi laki tatu. Vigumu sana kukamatwa,”
alisema.
GONGO INAVYOTENGENEZWA
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili ulibaini pombe hiyo
inatengenezwa kwa kutumia malighafi mbalimbali ikiwamo mapapai yaliyooza,
vitambaa vichafu vilivyovunda, mihogo na wakati mwingine kinyesi cha binadamu
hasa wakati bidhaa nyingine zinapoadimika.
Mfanyabiashara mmoja (jina linahifadhiwa) alisema
amekuwa akipika gongo na kuigawa katika madaraja matatu; iliyopikwa kwa mapapai
yaliyooza ndiyo inayopendwa zaidi na wateja wake ikilinganishwa na iliyotumia
malighafi nyingine.
“Sisi tunatumia mapapai yaliyooza, tunaongeza na sukari
pamoja na hamira, ikishaiva tunaitenga kutokana na madaraja yake. Gongo ya eneo
hili inasifika sana kwa sababu ya ubora wake, hatuna tatizo la ukosefu wa maji
kama walilonalo wenzetu ndiyo maana unaona tunaung’ang’ania huu mto hapa,”
alisema na kuongeza :
“Kama mapapai yakiadimika sana, tunaweza kupika kwa
kutumia vitambaa vichafu au mihogo.”
Akifafanua alisema wamekuwa wakitembea kwenye madampo
kuokota vitambaa pamoja na takataka nyingine, kisha huziloweka kwenye maji kwa
muda mrefu hadi zivunde ndipo huwa tayari kwa kupikia gongo.
Uchunguzi uliofanywa unaonyesha kuwa mbali ya pombe hiyo
kutengenezwa kwa kutumia takataka zinazookotwa kwenye madampo, pia huongezewa
ukali kwa kutumia dawa za kuongezea vitamini mifugo.
Mteja mmoja wa pombe hiyo ambaye alijitambulisha kwa
jina moja la Sadick, alisema gongo inayopikwa eneo hilo imekuwa maarufu kwa
kuwa kuna dawa ya mifugo ya Multivitamin ambayo huongezwa baada ya pombe hiyo
kuiva.
“Mimi ninafahamu kuna dawa ya mifugo inawekwa kwenye hii
gongo ili kuiongezea nguvu. Sijui ni dawa aina gani, lakini kuna jamaa huwa
namwona anakuja kuuza hiyo dawa. Gongo iliyowekwa hiyo dawa inakuwa na nguvu
sana,”alisema Sadick.
Mtaalamu wa Mifugo, Joseph Nong’ona alisema wanywaji wa
pombe hiyo wapo katika hatari ya kudhurika kiafya kwa kuwa dawa ya Multivitamin
inayotolewa kwa wanyama ina nguvu zaidi ikilinganishwa na ya binadamu, na
kwamba mtu haruhusiwi kunywa maziwa au nyama ya mnyama aliyepewa dawa hiyo kwa
siku tatu.
“Multivitamin anayopewa mnyama ina ‘concentration’ kubwa
ikilinganishwa na ile ya binadamu, lakini pia ikumbukwe kuwa ile ni kemikali
sijui inakuwaje inapochanganywa na gongo ambayo yenyewe tu ina madhara makubwa
kiafya. Kwa kawaida mnyama akipewa dawa hiyo huwa tunashauri asikamuliwe mazima
au nyama yake isitumike kwa siku tatu,” alisema Nong’ona.
Akizungumzia biashara hiyo, Katibu wa Mtaa wa Kilungule,
Juma Ahmed aliwatetea wafanyabiashara hao kwa madai kuwa hajawahi kupata
taarifa zozote za kufanya uhalifu badala yake wamekuwa walinzi wa amani katika
mtaa huo.“Ni watu wazuri sana, sijawahi kusikia wamefanya jambo lolote baya,
kwanza wamegeuka kuwa walinzi wa amani hapa mtaani kwetu… wanajua biashara
wanayoifanya siyo halali kwa hiyo hawataki matatizo na mtu,” alisema Ahmed.
Kamanda wa Polisi wa Temeke, Engelbert Kiondo alisema
suala la biashara ya gongo linatakiwa kudhibitiwa na jamii inayowazunguka
wafanyabishara hao kwa kutumia ulinzi shirikishi.
“Wanataka kuipa Polisi kazi bure tu, jamii ndiyo
inayohusika na suala hilo. Serikali ya mtaa kwa njia ya ulinzi shirikishi
wanaweza kuamua kwenda kuvunja mitambo ya gongo,” alisema Kiondo.
Akizungumzia tuhuma kuwa baadhi ya Polisi wanawalinda
wafanyabiashara wa gongo, Kiondo alisema tuhuma hizo zimekuwepo muda mrefu na
kwamba zimeshapitwa na wakati.
CHANZO: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment