![]() |
| Muandamanaji akiwa amebeba kiti na kisu wakati wa mapambano baina ya wafuasi na wapinzani wa rais aliyeondolewa madarakani Muhammad Mursi, Julai 3. |
Kabuga Kanyegeri
Utawala wa kijeshi nchini Misri uliyakandamiza vikali maandamano ya amani yaliyofanywa na wafuasi wa rais aliyendolewa madarakani, Muhammad Mursi, kwa kuwaua na kuwakamata mamia ya waaandamanaji hao mbele ya macho ya walimwengu.
Kwa mauaji haya, utawala huo ulionesha dhahiri kuwa matendo yao hayo ya ukatili yanauwekea kivuli utawala wa Husni Mubarak aliyeitawala nchi hiyo kwa miaka 30.
Namna utawala wa jeshi ulivyochukua madaraka na vitendo vyake vya umwagaji damu baada ya mapinduzi, kunawafanya watu wayafafanishe mapinduzi hayo na yale yaliyofanywa na Vuguvugu la Maafisa Huru mwaka 1952, yakiongozwa na Gamal Abdel Nasser, ambaye baadaye aliitawala nchi hiyo kwa kipindi cha miaka 16, dhidi ya Mfalme Farouk wa Misri. Akisadiwa na vuguvugu la Udugu wa Kiislamu (Muslim Brotherhood), Nasser alimuondoa Farouk madarakani, lakini baada ya kufanikisha mapinduzi alianzisha kampeni ya kulifutilia mbali vuguvugu la Udugu wa Kiislamu.
Msimamo kandamizi wa Nasser dhidi ya vuguvugu hilo uliendelezwa na wale waliokuja baada yake, na mbinyo huo uliendelea mpaka mwezi Februari 2011 baada ya utawala wa Mubarak kuanguka.
Hata hivyo, kutumia mbinu za Nasser kuwafuta Muslim Brotherhood hazitawasaidia watawala wa kijeshi. Kwa mazingira ya sasa haiwezekani kwa Wamisri waliopata demokrasia kurudi kwenye mapinduzi ya kijeshi. Watawala wa kijeshi hawana budi kujifunza kutoka kwa utawala wa Algeria. Yaliyofanywa mapinduzi dhid ya serikali ya Chama cha Ukombozi wa Kiislamu (FIS), kilichokuwa kimepata asilimia 80 ya kura katika uchaguzi mkuu wa mwaka 1991, ambao ndio uchaguzi wa kwanza wa kidemokrasia na wa uhuru, yaliitumbukiza nchi hiyo katika vita vya wenyewe kwa wenyewe na umwagazi damu uliodumu kwa muda mrefu.
Wakati uwepo wa tawi la kijeshi la chama hicho ukitumiwa na watawala wa kijeshi wa Ageria kama kisingizio, vuguvugu la Muslim Brotherhood halikutumia fujo wala mabavu, bali limekuwa likiandaa maandamano ya amani maeneo ya mijini ili wasiupe kisingizio utawala huo. Hawakuishia hapo, bali wameenda mbali zaidi na kutangaza kuwa hawatatumia ghasia na mabavu kudai haki yao.
Hata wale ambao mwanzo walionekana kuunga mkono utawala wa kijeshi, sasa wameanza kuukosoa baada ya mauaji iliyoyafanya. Wakati utawala huo ukidai kuwa wananchi wanauunga mkono, ukweli wa mambo ni tofauti kabisa.
Wamisri wanajua nini maana ya mauaji na umwagaji damu huu. Pia wanajua kwa nini Marekani, ambayo inalihonga jeshi la Misri dola trilioni 1.3 kila mwaka ili kuhakikisha usalama wa Israeli, imekaa kimya kuhusu janga hili.
Aliyekuwa Waziri wa Mashauri ya Kigeni wakati wa utawala wa Rais George W. Bush, Condoleezza Rice, alikiri kwamba walitelekeza sera potofu katika eneo la Mashariki ya Kati kwa kuziunga mkono tawala za kidikteta katika eneo hilo. Ni ngumu kuelewa kwa nini sera hizo hizo bado zinatekelezwa na utawala wa Obama, utawala ambao awali ulionekana kutuma ujumbe wa amani duniani na kutaka kuonesha sura tofauti na mtangulizi wake.
Marekani haiwezi kukaa tu na kuona maendeleo ya kidemokrasia yakipatikana katika eneo la Mashariki ya kati iwapo maendeleo hayo yanahatarisha uhai na usalama wa Israeli.
Kadhalika, tumeiona Jumuiya ya Umoja wa Ulaya ikitoa matamko legelege, kama vile: “Tunahuzunika na tunafuatilia kwa karibu mambo yanavyoendelea nchini Misri.”
Ukweli ni kwamba utawala wa kijeshi huawezi kuwa na nguvu bila kuungwa mkono na madola ya Magharibi. Wamisri hawakubaliani na maamuzi na matendo yote yanayofanywa na Muslim Brotherhood, lakini baada ya uzoefu wa miaka 69, wanajua maana ya utawala wa kijeshi. Ndiyo maana walifanya uasi dhidi ya utawala wa kijeshi uliokaa madarakani kwa muda wa mwaka mmoja na nusu baada ya kuanguka kwa utawala wa Mubarak na kuwalazimisha kufanya uchaguzi wa kidemokrasia.
Watawala wa kijeshi, mabaki ya utawala wa Mubarak na baadhi ya wafanya biashara wanafanya juhudi kubwa kuyageuza mapinduzi hayo kuwa mapinduzi ya kisasi. Lakini wanaweza kufanikiwa? Hapana, hawataweza.
Kwa sababu, iwe sasa au baadaye, wananchi wa Misri watabaini kuwa watawala wa kijeshi hawapo kwa maslahi ya nchi, bali wanataka kuurejesha utawala wa Mubarak. Na hilo limeshafanywa na watawala hao. Viongozi wa utawala wa zamani wameteuliwa na kurejeshwa kwenye nyadhifa zao zilezile za zamani au nyadhifa bora zaidi.
Watawala wa kijeshi hawawezi kufanya miujiza ya kuipa Misri mito ya maziwa na kubadilisha mkondo wa matukio. Kwa hivyo, watawala hao ambao waliahidi kuwa wasingewashambulia wanaofanya maandamano ya amani baada ya mapinduzi, wanapaswa kuacha kuwashambulia wafuasi wa Muslim Brotherhood na watetezi wa demokrasia.
Uaminifu na uadilifu wa jeshi la Misri ni muhimu sana kwa Wamisri kwa sababu matukio yanayoendelea katika eneo la Mashariki ya kati yanahitaji jeshi imara lililo huru na lisilokuwa na upendeleo.

0 comments:
Post a Comment