DALILI 15 ZA MAREKANI KUISHAMBULIA KIJESHI SYRIA

 



Kabuga Kanyegeri

Imeelezwa kuwa utawala wa Rais Obama unafikiria kuishambulia Syria japokuwa wananchi wengi wasingependelea kuiona nchi yao ikiingia katika vita nyingine. Obama hatapata idhini ya Bunge la Congress kuanzisha vita yoyote, na hatapata idhini ya Umoja wa Mataifa kwa sababu azimio lolote la aina hiyo litazuiliwa na Urusi. Yaonekana hili litakuwa pigo kubwa kwa sera ya nje ya Marekani.

Hoja ya kuishambulia Syria imeshawekwa mezani kwa sababu ya shambulizi la silaha za kemikali lilitokea wiki iliyopita katika eneo la jirani na mji wa Damascus lililowaua watu wapatao 1,400. Utawala wa Rais Obama na baadhi ya mataifa ya Magharibi wanautupia lawama utawala wa Assad kwa shambulizi hili.

Lakini, wengine wanaona kuwa haingii akilini kwa utawala wa Assad kufanya jambo kama hilo. Kwanza, utawala huo unaonekana kushinda vita, na Assad anajua vema kuwa Obama ameshasema kwamba matumizi ya silaha za kemikali nchini Syaria utakuwa “msitari mwekundu” kwa Marekani.

Hivyo basi, kwa nini utawala wa Assad ufanye shambulizi la kinyama kama hilo dhidi ya wanawake na watoto mita chache kutoka mahali walipo wachunguzi wa Umoja wa Mataifa?

Kwa nini Assad ajiweke hatarini kuingia vitani na Marekani na washirika wake wa NATO?

Assad atakuwa mtu wa ajabu sana kufanya unyama na mauaji ya kutisha kama hayo na yasiyokuwa na tija katika mapambano yake.

Baadhi ya wafuatiliaji wa mambo wanaona kuwa watakaonufaika na shambulizi hili la silaha za kemikali ni waasi. Kuna uwezekano mkubwa wa majeshi ya nje kuingia moja kwa moja nchini Syria.

Nina imani huwenda tusijue kabisa ukweli wa nani hasa aliyehusika au kuwa nyuma ya shambulizi hiyo. Na hata kama lisingetokea, Marekani na NATO wangekuja na kigezo kingine cha kuingia vitani. Wanaonekana kuazimia kabisa kumalizana na Assad, lakini sina hakika kama wameyafikiria madhara ya hatua yao hiyo.

Zifuatazo ni dalili 15 za kwamba Obama ameshaamua kuingia vitani na Syria…

1.     Syria imewakubalia na kuwaruhusu maafisa wa Umoja wa Mataifa kwenda kufanya uchunguzi kwenye eneo yalipotokea mashambulizi ya silaha za kemikali yaliyowaua watu 1,400, lakini “afisa mmoja mwandamizi wa Marekani” anasema kuwa uchunguzi huo “umechelewa mno na hivyo hauwezi kuaminika”.  

2.    Kwa mujibu wa kituo cha habari cha ABC News, Ikulu ya Marekani inasema kuwa kuna “shaka ndogo sana” kwamba Utawala wa Assad ulihusika na shambulizi hilo baya lililotokea wiki iliyopita.  

3.    Manowari nne za Marekani zenye makombora ya masafa zinasogea kwenye eneo maalumu katika Bahari ya Mediterrania. Amri itakapotolewa, zitaweza kuishambulia Syria ndani ya dakika kadhaa.

Maafisa wa ulinzi wa Marekani wameliambia shirika la habari la Associated Press kuwa jeshi la wanamaji la nchi hiyo limetuma manowari ya nne yenye makombora ya masafa kwenye Bahari ya Mediterrania lakini hawajapewa amri ya moja kwa moja kuishambulia Syria.

Meli za jeshi la wanamaji la Marekani lina uwezo wa kuchukua hatua mbalimbali za kijeshi, ikiwa ni pamoja na kutuma ndege zenye silaha aina ya Tomahawk, kama walivyofanya Libya mwaka 2011 kama sehemu ya kampeni ya kijeshi ya kimataifa iliyoiangusha serikali ya Libya.

4.    Kituo cha habrai cha CBS kimeripoti kuwa “Pentagoni inafanya maandilizi ya awali kwa ajili ya mashambulizi ya makombora dhidi ya vikosi vya serikali ya Syria.”  

5.    Siku ya Jumamosi, Rais Barack Obama alikutana na timu ya usalama wa taifa kujadili hatua zinazotakiwa kuchukuliwa nchini Syria.  

6.    Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Chuck Hagel, anasema kuwa Rais Barack Obama amemtaka “kuandaa hatua mbalimbali za dharura” kwa kadiri mgogoro wa Syria utakavyokuwa.  

7.    Baada ya kuzungumza kwa simu na Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron kuhusu hali ilivyo nchini Syria, Ikulu ya Marekani ilitangaza kuwa viongozi hao walielezea “kuguswa mno” na shambulizi la silaha za kemikali lililotokea wiki iliyopita.  

8.    Makamanda wa kijeshi kutoka Marekani, Uingereza, Saudi Arabia, Qatar, Uturuki, Ufaransa, Italia na Canada wanakutana mjini Amman, nchini Jordan siku ya Jumapili kuratibu mipango ya mshambulizi yajayo dhidi ya Syria.  

9.    Kwa mujibu wa gazeti la pili kwa ukubwa nchini Ufaransa, vikosi vya waasi vinavyodaiwa kupewa mafunzo na CIA vimekuwa vikiingia kwa wingi nchini Syria “tangu katikati mwa mwezi Agosti”.

Kuna taarifa kuwa wapinzani wa serikali, wanaosimamiwa na makomandoo wa  Jordan, Israeli na Marekani wamekuwa wakiingia Damascus tangu katikati mwa mwezi Agosti. Hii inaweza kuwa sababu ya rais wa Syria kutumia silaha za kemikali.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka gazeti la Le Figaro, kikosi cha kwanza kilichopatiwa mafunzo ya kivita na Wamarekani nchini Jordan kinaelezwa kuwa kimeanza kazi katikati ya mwezi Agosti kusini mwa Syria, katika mkoa wa Deraa. Kundi la kwanza la askari 300, wanaoelezewa kuungwa mkono na makomandoo wa Israeli na Jordan, na pia CIA, walivuka mpaka Agosti 17. Kundi la pili liliingia tarehe 19.

10. Jeshi la Marekani lilipeleka idadi kubwa ya ndege aina ya F-16 kuelekea Jordan mapema mwaka huu kwa ajili ya mazoezi ya kijeshi, lakini ndege hizo zikabaki huko “kwa ombi la serikali ya Jordan.”

11. Kwa mujibu wa nyaraka za siri zilizochapishwa na mtandao wa WikiLeaks mapema Machi 2012, NATO ilipeleka watu maalumu ndani ya Syria kuandaa mabadiliko ya utawala tangu mwaka 2011.

12. Gazeti la The Times la Israeli limeripoti kuwa tathmini ya ndani ya kijeshi imeeleza kuwa “Marekani inafikiria kwa uzito mkubwa shambulio la muda mfupi lakini lenye taathira litakalouonesha utawala wa Damascus kuwa jumuiya ya kimataifa haitavumilia matumizi ya silaha za maangamizi dhidi ya raia au viashiria vingine vyovyote.”

13. Seneta wa Marekani, John McCain, hivi karibuni alisema kuwa jeshi la Marekani lisipoipiga Syria itakuwa kama “kuwaruhusu madikiteta wengine makatili duniani kama wanataka kutumia silaha za kemikali.  

14. Kwa mujibu wa gazeti la New York Times, “mashambulizi ya anga yaliyofanywa na NATO huko Kosovo” yanadurusiwa “ kama ishara ya kuchukua hatua bila kupata kibali kutoka Umoja wa Mataifa.”


15. Ikulu ya Marekani imetoa taarifa kwamba utawala wa Rais Obama hauna mipango ya “kuvaa mabuti,” (yaani kupeleka askari wa ardhini)  lakini haikuondoa uwezekano wa aina nyingine za hatua za kijeshi.

Kwa maoni na ushauri:

+255 712 566 595
Share on Google Plus

About mahamoud

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment