Na Kabuga kanyegeri
Mwaka 2009, Rais wa Marekani Barack Obama alitangaza kuona “mabadiliko” katika uhusiano wa nchi yake na Urusi. Kwa bahati mbaya, mabadiliko haya hayajatokea kabisa.
Zaidi ya miongo miwili baada ya Vita Baridi kufikia kikomo, Urusi inaendelea kuiona Marekani kuwa ni mbabe na mnafiki, ikiamini kuwa Washington inataka kuitenga Urusi katika kila fursa. Wakati huo huo, Marekani bado haijawa na utayari wa dhati kabisa wa kuikubali Urusi kama dola muhimu kieneo na kimataifa, badala yake inaiona kama dola ya kiimla yenye kukwamisha na kuitatiza mipango ya Marekani.
Kumekuwepo na ukunjufu ‘kiduchu’ kwa nchi moja kushughulikia matatizo ya mwenzake. Ukiangalia lugha ya mwili iliyooneshwa na viongozi wa mataifa hayo kwenye mkutano wa kilele wa hivi karibu wa G8, baada ya Urusi kuikasirisha Washington kwa kukataa kushikamana na sera yake juu ya Syria, ni ishara tosha kwamba siku hizi viongozi hao hawapendani.
Pigo la hivi karibuni kabisa kwenye uhusiano wa nchi hizo limetokea mapema wiki jana baada ya Urusi kutoa hifadhi ya mwaka mmoja kwa bwana Edward Snowden, aliyekuwa amekwama katika uwanja wa ndege wa Sheremetyevo mjini Moscow akitokea Hong Kong tarehe 23 Juni. Snowden anatafutwa na mamlaka za Marekani kwa tuhuma za kuvujisha siri nyeti za shughuli za ujasusi zinazofanywa na Marekani. Uamuzi huo umekuja wiki mbili tu baada ya Rais wa Urusi, Vladimir Putin kuusifu uhusiano wa nchi yake na Marekani, akisema kuwa uhusiano huo ni muhimu zaidi kuliko kashfa yoyote ya kijasusi. Kwa kweli Urusi inaonekana kudhani kuwa “mambo yataendelea kuwa kawaida,” na kwamba tukio hilo halitaathiri uhusiano wao hata kidogo.
Lakini Marekani haikubali. Imeeleza kuwa imehuzunishwa mno na uamuzi wa Urusi inaoamini kuwa “unadhoofisha ushirikiano wa muda mrefu” katika masuala ya kisheria. Hata hivyo, mashirika na taasisi za haki za kibinaadamu, kama vile shirika la Human Rights Watch, yana mtazamo tofauti, wakieleza kuwa Snowden alikuwa na madai ya msingi na kwamba “sheria za Marekani hazitoi ulinzi wa kutosha kwa wanaovujisha siri pindi linapohusika suala la siri nyeti.”
Marekani ilikuwa na nafasi ya kulishughulia vizuri suala hili. Kwa bahati mbaya haikulishughulia kwa namna nzuri, hususan uamuzi wake wa kuwataka washirika wake wa nchi za Ulaya kuishusha ndege ya Rais wa Bolivia, Evo Morales, kwa kile walichoamini kuwa Snowden alikuwa ndani ya ndege hiyo. Marekani inaweza kuwa taifa lenye nguvu zaidi duniani, lakini sio polisi wa dunia. Hili ni jambo ambalo lilibua mivutano zaidi na Urusi na kuwakasirisha majirani zake wa nchi za Amerika ya Kusini. Hivyo, yumkini uamuzi wa Urusi ulikuwa kama jibu kwa jinsi Marekani ilivyolishughulikia sakati hilo na kutaka kuonesha misuli yake.
Suali lililopo sasa ni hatua ipi itakayochukuliwa na Marekani? Baadhi ya maseneta wamekasirishwa sana na kitendo hicho cha Urusi. Seneta mtata, John McCain, ni miongoni mwa waliotoa kauli nzito na kali dhidi ya Urusi, akiorodhesha hatua zinazoweza kuchukuliwa na Marekani kulipiza kisasi. Alienda mbali zaidi kiasi cha kutoa wazo la kufanya kikao cha haraka cha Umoja wa kujihami wa nchi za Magharibi, NATO, kuchukua hatua ya makusudi ya kupanua wigo wake kwa kuipa Georgia uanachama rasmi, huku ikizingatiwa kuwa Urusi inalipinga suala hilo, jambo lililojidhihirisha katika mgogoro wa mwaka 2008 baina ya Urusi na Georgia.
Hata hivyo, wakati kumekuwepo na wito wa kuutafakari upya uhusiano na Urusi inayoongozwa sasa na Putin, inaonekana kuwa mchafukoge wa uhusiano huo hautakuwa na maslahi kwa pande zote mbili, na hakuna upande ambao ungependa kuona uhusiano huo ukizidi kuvurugika. Urusi ina nafasi muhimu kwenye uwanda mpana zaidi wa masuala muhimu yanayohusu usalama wa Marekani, maendeleo na ushawishi wa kimataifa. Nchi zote mbili ni wachezaji muhimu katika kanda zote mbili, ile ya Ulaya – Atlantiki na Asia-Pasfiki, na zina uwezo wa kipekee katika kuelekeza changamoto za kidunia kama vile mabadiliko ya tabia nchi, suala la Iran, Afghanistan, usalama wa mitandaono, n.k.
Kwa muktadha huo, ninaamini kuwa litakuwa kosa kubwa kuruhusu uhusiano baina yao kuendelea kutazamwa katika ‘tundu’ finyu la sakata la Snowden. Obama asifikirie kuacha kuhudhuria kikao muhimu baina ya Marekani na Urusi kilichopangwa kufanyika hivi karibuni katika mji wa St. Petersburg. Katika hali kama hii, kukatisha mawasiliano kutazorotesha zaidi hali hii, na ninaamini Obama atakuwa makini kuliangalia na kulitafakari jambo hili.

0 comments:
Post a Comment