Mafuriko makubwa yaliyotokana na mvua kali yamesababisha vifo vya watu wapatao 170 nchini Afghanistan na nchi jirani ya Pakistan.
Maafisa wa Afghanistan wanasema kuwa zaidi ya watu 60 wamepoteza maisha katika wilaya ya Sarobi, umbali wa saa moja kutoka mji mkuu wa nchi hiyo, Kabul. Kwa uchache watu 24 pia wamepoteza maisha na zaidi ya nyumba na maduka 100 kuharibiwa katika majimbo ya mashariki mwa Afghanistan.
Na huko Pakistan, mafuriko makubwa yaliyotokana na mvua kali yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 80.
Jimbo la Kashmir, majimbo ya Punjab, kusini magharibi mwa Balochistan na kusini mwa Sindh ni miongoni mwa maeneo yaliyoathiriwa zaidi na mafuriko hayo. Inaelezwa kuwa hali ni mbaya. hususan katika mji mkubwa zaidi nchini humo wa Karachi, kwa sababu ya mfumo mbovu wa miondombinu ya maji taka na mifereji.
Mara kwa mara Pakistan hukumbwa na mafuriko makubwa katika msimu wa mvua kali ambao hutokea mwezi Julai na Agosti. Mwaka 2010 nchi hiyo ilikumbwa na mafuriko mabaya zaidi katika historia yake yaliyoua zaidi ya watu 1,700.
0 comments:
Post a Comment