Maafisa wa Tume ya Uchaguzi nchini Zimbabwe wametangaza kuwa Rais Robert Mugabe ametetea kiti chake baada ya kushinda katika uchaguzi wa urais uliofanyika wiki hii kwa kupata asilimia 61 ya kura zote. Ushindi huo ni pigo kubwa kwa kambi ya upinzani iliyoapa kwenda mahakamani kuonesha kuwa uchaguzi huo haukuwa huru na wa haki.
Leo aliyekuwa Waziri Mkuu na kiongozi wa zamani wa chama cha wafanyakazi, Morgan Tsvangirai alisema kuwa chama chake kitapinga matokeo ya uchaguzi aliyoyaita kuwa ni “fedheha.” Uchaguzi wa Jumatano ulikuwa pigo kubwa kwa bwana Tsvangrai mwenye umri wa miaka 61 dhidi ya Rais Mugabe mwenye umri wa miaka 89 na ambaye ametawala kwa miaka 33 tangu Zimbabwe ilipojipatia uhuru wake.
Waziri Mkuu wa Zimbabwe, Morgan Tsvangirai alisema kuwa chama chake kitaenda mahakamani kupinga ushindi wa chama cha Rais Robert Mugabe cha ZANU-PF.
Ushindi huo wa Mugabe unakuja baada ya matokeo ya mapema kuonesha kuwa chama chake cha ZANU-PF, kimeshinda theluthi tatu ya viti vya ubunge, na hivyo kuwa na nguvu ya kufanya mabadiliko kwenye katiba mpya iliyopitishwa hivi karibuni. ZANU-PF kinasema kuwa watu milioni 3.95 walipiga kura katika uchaguzi wa Jumatano.
“Nina furaha sana kwamba uchaguzi umefanyika kama ulivyotarajiwa… ulikuwa wa amani, huru, wa haki na wazi,” alisema Waziri wa Ulinzi ambaye pia ni mwanachama wa ZANU-PF, Emmerson Mnangagwa.
“Hatua inayochukuliwa na MDC itaifanya nguvu yao ya kisiasa inazikwa moja kwa moja.”
Wakati viongozi wa chama cha ZANU-PF wakishangilia, Morgan Tsvangirai, akizungumza kutoka kwenye makazi ya Waziri Mkuu baada ya matokeo rasmi, alisema kuwa kama uchaguzi ungekuwa umefanyika kwa haki, chama chake kingeshinda.
“Hili limeirudisha Zimbabwe kwenye mgogoro wa kisiasa, kikatiba na kiuchumi,” alisema Tsvangirai. “Uchaguzi huru na wa haki unapaswa kufanyika mapema iwezekanavyo. Hatuupingi uchaguzi huu eti kwa sababu chama cha MDC hakikushinda, bali kwa sababu uchaguzi ulijaa udanganyifu.”
Bwana Tsvangirai alisema chama chake kitatumia njia za kisheria kupinga uchaguzi huo na wakati huo huo kuwataka watu wasifanye ghasia na vurugu. Katiba inawapa wananchi siku saba za kuwasilisha malalamiko yao mbele ya mahakama ya kikatiba. Iwapo hakuna malalamiko yoyote au malalamiko husika yakitupiliwa mbali, rais ataapishwa ndani ya siku tisa baada ya matokeo rasmi kutangazwa.
Radiamali ya vyama hivyo viwili dhidi ya matokeo hayo itakuwa muhimu sana kwa Zimbabwe, uchumi wake na utawala wake. Waangalizi wa uchaguzi na Bwana Tsvangirai wamewataka watu kudumisha utulivu ili kuepuka yasijirudie yaliyotokea katika uchaguzi wa mwaka 2008 ambapo kwa uchache watu 200 walipoteza maisha yao katika ghasia zinazohusiana na uchaguzi, jambo lililoongeza matatizo katika uchumi ambao tayari ulikuwa taabani kutokana na ukosefu wa ajira na mfumo wa bei ulioshtadi.
Anguko la uchumi lilikoma mwaka 2009 baada ya serikali kuacha kutumia safari ya nchi hiyo na kuanza kutumia dola ya Marekani na kuunda serikali ya umoja Mugabe akiwa kama rais na Bwana Tsvangirai kama waziri mkuu. Leo bwana Tsvangirai aliweka bayana kuwa hayuko tayari kuingia katika serikali nyingine ya ushirika na atakaa pendekezo lolote kutoka ZANU-PF litakalomtaka kufanya hivyo.
Polisi walionekana kuwa katika hali ya tahadhari kubwa, wakifanya doria katika barabara kuu zinazoelekea katika mji mkuu Harare huku wakiyakagua magari kuhakikisha kama yamebeba silaha.
“Uchumi wetu sasa utakuwa matatani,” anasema Jongwe MacDonald mwenye umri wa miaka 28, akiwa amekaa nyuma ya duka mjini Harare. “Tulitaka Tsvangirai shinde na ili wahisani waje Zimbabwe kusaidia. Tulitaka mabadiliko.”
Leo Bwana Tsvangirai alikariri wasiwasi wake juu ya kile alichosema kuwa ni udanganyifu alioushuhudia wakati wa uchaguzi, ambao ulijumuisha wapiga kura waliokuwa na vyeti bandia, watu kupakiwa kwenye mabasi na kupelekwa sehemu mbalimbali kuipigia kura ZANU-PF na wapiga kura wengi ambao hawakupiga kura kwa sababu majina yao hayakuwepo kwenye orodha ya wapiga kura. Wasemaji na maafisa waandamizi wa ZANU-PF walikanusha tuhuma zote hizo.
Siku ya Ijumaa waangalizi kadhaa walioruhusiwa na Mugabe kuingia nchini walithibitisha malalamiko mengi yaliyotolewa na Tsvangiria lakini walisema kuwa kiujumla mchakato wa upigaji kura ulikuwa huru na haukuwa na vitisho vilivyoshuhudiwa katika chaguzi zilizopita. Umoja wa Afrika ulisema kuwa japo kulikuwa na masuala kadhaa kuhusu uchaguzi huo kama vile idadi kubwa ya watu ambao hawakuweza kupiga kura kutokana na majina yao kutoonekana, bado hawakuona kitu ambacho kingeufanya uchaguzi huo kuwa batili. Wakati huo huo, Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika, SADC, ilimtaka bwana Tsvangirai kuyakubali matokeo hayo, hata kama “yanaumiza.”

0 comments:
Post a Comment