‘PAKA ANAPOKUWA PANYA’





Na Kabuga Kanyegeri

“Tulimchagua [Mohammed] Mursi, sio baraza la kijeshi,” anasema mwanamke mmoja katika Medani ya Msikiti wa Rabaa al-Adawiya.

Analielekeza swali lake rahisi sana kwenye kipaza sauti cha kamera ya televisheni kilichokuwa kimeelekezwa kwake. Anauliza nani aliyeiba kura yake? Swali hili analielekeza kwenye jumuiya ya Kimataifa, Marekani na Jumuiya ya Umoja wa Ulaya.

Kila mtu analijua jibu la swali hili.

Hapa kuna jambo moja rahisi sana linalojitokeza. Kila kitu sasa kimekuwa wazi mbele ya macho yetu. Jambo lenyewe ni kuwa, Rais aliyechaguliwa kidemokrasia aling’olewa na jeshi. Hiki ndicho chanzo cha yale yote yanayoendelea nchini humo. Ubaya wa mapinduzi haya ya kijeshi unatakiwa kueleweka na kuwekwa wazi.

Viongozi wote waliochaguliwa kidemokrasia hufanya makosa kwa namna moja ama nyingine. Utendaji wa kidemokrasia wa Mursi ni jambo ambalo linahitaji kujadiliwa. Lakini hakumwaga damu wala kuanzisha utawala ambao kimfumo ulikiuka haki za binaadamu. Tunapaswa kuhoji iwapo kweli alitumia vibaya madara aliyokabidhiwa. Kwa kweli, ingawa alikuwa na makosa ya hapa na pale kama kiongozi, lakini hakuna kosa lake hata moj linalohalalisha mapinduzi.

Madikteta wote katika Ulimwengu wa Kiislamu “waliyakaribisha” mapinduzi haya. Walikuwa na hofu kama ile iliyowahi kuwakumba wafalme wa Ulaya walipoyahofia mapinduzi wa Ufaransa. Waliyakandamiza mapinduzi hayo kuanzia kwenye shina kiasi kwamba walimwaga misaada na pesa kwa walaghai na matapeli waliowaunga mkono.

Ni rahisi sana kuelewa kile kilichowasukuma kuchukua hatua hiyo. Lakini msiba mkubwa ni pale Marekani na Umoja wa Ulaya, wapiganiaji wa demokrasia na haki za binaadamu, walipoamua kuufumbia macho uhalifu huu uliofanywa na walaghai wa madaraka huku ulimwengu mzima ukishuhudia na kuwaunga mkono majenerali waliofanya mapinduzi hayo. Waziri mmoja wa Ufaransa aliwahi kusema, “kwetu tnamuita paka kuwa ni paka,” lakini ajabu ni kuwa Ufaransa ilishindwa kuyaita mapinduzi kuwa ni mapinduzi. Hakuna kiongozi wao yeyote aliyeweza kutamka kuwa “mapinduzi ni mapinduzi”. Walianza kukwepa na kuchanganya mambo ili kuepuka natija ya kimaadili na kisheria ya kuyaita mapinduzi kuwa ni mapinduzi.

Tofauti na Umoja wa Afrika (AU) na nchi chache, hakuna aliyeliona jambo hilo kuwa lenye ukakasi.

Inasemekana kuwa mtu hufanya kosa katika mojawapo ya njia mbili: ima akiwa ameyafumbua macho yake au akiwa ameyafumba. Hili linzihusu hata serikali pia. Umoja wa Ulaya unajaribu kumshawishi Mursi “kushirikiana” na utawala wa kijeshi na waziri wa mambo ya nje wa Marekani anawataka wale waliowaua waandamanaji 200 waliokuwa wakiandamana kwa amani wajifanyie “uchunguzi huru na usiokuwa na upendeleo.”

Kwa muktadha huo wanauhalalisha utawala wa wanyang’anyi huku wakijifanya kuunga mkono demokrasia. Malale haya yako wazi kiasi kwamba hayawezi kujificha nyuma ya pazia la siasa safi.



Hata hivyo, kuna uwezekano mkubwa kwamba uhusika wa Marekani hauishii tu kushindwa kuyaita mapinduzi hayo kuwa ni mapinduzi, hususan ikizingatiwa kuwa inaendeleza uhusiano wa karibu na jeshi la Misri na hivyo inaweza kuwa na ushawishi mbaya.

Je, wale wanaoyanga mkono mapinduzi hayo kwa siri au dhahiri, wale wanaoshindwa kuyataja kama mapinduzi na wale wanaoyahalalisha kwa njia moja au nyingine, hawaioni rangi nyekundu mikononi mwao?

Hapo mwanzoni mapinduzi yalitakiwa kuungwa mkono kwa kusimama katika Medani ya Tahrir lakini kwa sasa yanatakiwa kuungwa mkono kwa kusimama katika Medani ya al- Adawiya. Kwa sababu, leo hii, sauti zinazotaka haki zinavuma kutoka medani ya Adawiya.

“Medani haitengenezi watu; watu hutengeneza medani,” aliongeza kusema mwanamke huyo niliyemtaja mwanzo. Yumkini anachojaribu kufanya hapa ni kuwafanya wale wanaotangaza maandamano ya Medani ya Tahrir kwa kuyapuuza maandamano ya medani ya Al-Adawiya, ambayo ni kitovu cha upinzani dhidi ya mapinduzi ya kijeshi, watambue kuwa medani na maandamano ya kweli yapo katika Medani ya Msikiti wa Rabaa al-Adawiya.


Share on Google Plus

About mahamoud

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment