WATU 130 WAPOTEZA MAISHA KATIKA MAPIGANO NCHINI KONGO

Waasi wa M23





Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imetangaza kuwa mapigano baina ya vikosi vya jeshi la Serikali na waasi mashariki mwa nchi hiyo yamesababisha vifo vya watu wasiopungua 130, wakiwemo wanajeshi 10. 


“Vikosi vyetu vimewasababishia hasara nzito wapiganaji wa M23, miongoni mwao 120 wameuawa na 12 wamekamatwa," msemaji wa serikali Lambert Mende leo hii, akielezea mapambano yaliyozuka mwishoni mwa juma.


Mende aliongeza kusema kuwa mapigano hayo yaliyozuka jana Jumapili katika Jimbo la Kivu ya Kaskazini baina ya jeshi la Kongo na waasi wa M23 yalisababisha vifo vya askari 10.


Aliendelea kusema kuwa idadi kamili ya vifo kutokana na mapigano hayo haijawa wazi, akisisitiza kuwa "mpaka sasa vikosi vya jeshi vimejibu vikali mashambulizi haya.”

Msemaji huyo wa serikali aliendelea kusema kuwa vikosi vya jeshi vilifanikiwa kukamata maeneo yaliyokuwa yakishikiliwa na waasi baada ya kukimbia.


Ripoti zinasema kuwa askari 2,000 walitumika katika mapigano hayo. Hata hivyo, Mende hakuthibitisha idadi hiyo.


Hivi karibuni, askari wapatao 3,000 wa Umoja wa Mataifa walipelekwa katika eneo hilo. Askari hao wanaotoka katika nchi za Malawi, Afrika Kusini na Tanzania, wanaungana na askari wapatao 17,000 wa Umoja wa Mataifa ambao wameshatumwa katika eneo hilo.


Wakati huo huo, jana Jumapili, Shirika la Msalaba Mwekundu nchini Uganda lilisema kuwa zaidi ya wakimbizi 60,000 kutoka Kongo wamevuka mpaka na kuingia nchini Uganda tangu Julai 11 wakikimbia mapigano baina ya jeshi la Kongo na kundi la waasi wa Uganda katika mji wa mpakani.


Makundi kadhaa yenye silaha, ikiwemo M23, wanaendesha harakati zao za uasi mashariki mwa Kongo na wanapigania kuidhibiti nchi hiyo kubwa yenye maliasili za madini, kama vile dhahabu, urani, coltan, ambayo hutumika katika utengenezaji wa vifaa vingi vya elektroniki, ikiwemo simu za mkononi.



Tangu mwezi Mei 2012, takriban watu milioni 3 wameyekimbia makazi yao katika eneo la mashariki mwa Kongo. Takriban watu milioni 2.5 ni wakimbizi wa ndani, huku zaidi ya watu 460,000 wamekimbilia katika nchi za Rwanda na Uganda.
Share on Google Plus

About mahamoud

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment