KIONGOZI WA CHAMA CHA KIISLAMU BANGLADESH AHUKUMIWA KIFUNGO CHA MIAKA 90

In this photograph taken on May 13, 2012, Jamaat-e-Islami party


Mahakama maalumu nchini Bangladesh imemhukumu Ghulam Azam, kiongozi wa zamani wa chama cha Jamaat-e-Islami kwa tuhuma za kupanga mauaji wakati wa vita vya kupigania uhuru wa nchi hiyo kutoka kwa Pakistan mwaka 1971.


Duru kutoka mahakama ya Bangladesh zinasema kuwa Azam amehukumiwa kifungo cha miaka 90 jela kwa kuhusika katika mauaji ya umati wakati wa vita hivyo.


“Alikutwa na hatia isiyokuwa na shaka katika mashitaka yote matano. Mahakama iliona kuwa alistahiki adhabu ya kifo," alisema naibu mwanasheria mkuu M.K. Rahman.

Mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 90 alikanusha mashitaka yaliyotolewa dhidi yake na wafuasi wake wanasema kuwa mashitaka hayo yana msukumo wa kisiasa.


Baada ya hukumu hiyo iliyotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai nchini Bangladesh (ICT), ghasia ziliibuka baina ya polisi na wafuasi wa Azam. 

Makundi na taasisi kadhaa za haki za Binadamu wanasema kuwa mahakama iliyomhukumu Azam haina viwango vya kimataifa.

Mahakama hiyo maalumu imeshatoa hukumu zisizopungua tatu dhidi ya wanachama wa chama hicho, ikiwa ni pamoja na adhabu za vifo kwa makamu wa rais wa chama hicho na mwanachama mmoja wa zamani.

 
Mpaka sasa viongozi wa juu wa chama hicho wameshatiwa hatiani na mahakama hiyo kwa kuhusika na mauaji ya umati wakati wa vita hivyo, ambavyo vilisababisha iliyokuwa Pakistan ya Mashariki kujitenga na Islamabad.

Hatua hii inakuja katika hali ambayo upinzani unaituhumu serikali kutaka kuwatisha na kuwadhoofisha kwa kuwashitaki viongozi wao kwa tuhuma za makosa ya vita yaliyofanywa miaka 40 iliyopita.



Watu wamemiminika mara kadhaa katika mitaa ya mji wa Dhaka na baadhi ya miji mingine kuonesha upinzani wao dhidi ya mashitaka na hukumu zenye utata zinazotolewa dhidi ya wanaharakati na viongozi wa upinzani.


Zaidi ya watu 150 wamepoteza maisha katika makabiliano na polisi tangu mwanzoni mwa mwaka huu.


Chama Kikuu cha upinzani nchini Bangladesh cha BNP na makundi kadhaa ya Kiislamu wamefanya maandamano kadhaa ya kitaifa kupinga vikali 'mauaji ya kikatili' dhidi ya waandamanaji yaliyofanywa na vikosi vya usalama kwa miezi kadhaa iliyopita.


Bangladesh imekumbwa na masaibu mbalimbali katika historia yake, kama vile mapinduzi ya kijeshi, ghasia za umwagaji damu  na majanga ya asili.
Share on Google Plus

About mahamoud

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment