WAZIRI Mkuu wa Uturuki, Recep Tayyip Erdoğan amesema kuwa anamhesabu Muhammad Mursi, aliyeondolewa madarakani na jeshi mapema mwezi huu, kuwa ni rais wa Misri.
“Kwa sasa, rais wangu nchini Misri ni Mursi kwa sababu alichaguliwa na wananchi. Hivyo, tusipokuwa na msimamo kama huu, tutakuwa tumewapuuza na kuwadharau watu wa Misri. Kuudharau utashi wa wananchi wa Misri ni sawa na kujidharau wewe mwenyewe kwa sababu hapa Uturuki tunaheshimu utashi wa wananchi. Tungeuheshimu utawala wa mapinduzi ya jeshi kama wangekuwa wameshinda kwenye sanduku la kura,” alisema Erdoğan wakati wa chakula cha futari.
Akieleza kuwa jukumu la jeshi sio kutawala nchi, Erdoğan alibainisha kuwa jukumu pekee la jeshi ni kulinda mipaka ya nchi.
“Kwa nini kuna sanduku la kura? Kutokana na mtokeo ya kura, serikali itapatikana kwa utashi wa wananchi na serikali hiyo ndiyo itakayotawala nchi. Serikali hiyo inaweza kuwa na mafanikio au isifanikiwe. Serikali isipofanikiwa, kwa mara nyingine litaletwa sanduku la kura. Hapo ndipo utakapoweza kusema kuwa serikali imeshindwa,” alisema Erdoğan.
Erdoğan alibainisha kuwa baadhi ya mataifa ya nje hayakuisaidia kifedha serikali ya Mursi wakati wa kipindi cha urais wake uliodumu kwa muda wa mwaka mmoja; lakini, nchi hizo hizo zimeahidi kutoa dola bilioni 16 kuupa utawala wa kijeshi nchini Misri.
Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu na Kuwait zimeshatoa jumla ya dola bilioni 12 kuipa Misri baada tu ya kilichotokea hivi karibuni nchini humo.
Erdoğan, ambaye alilikosoa vikali jeshi la Misri kwa kumuondosha madarakani kiongozi aliyechaguliwa kidemokrasia, alikumbushia kuwa huko nyuma Uturuki iliwahi kukumbwa na mapinduzi kama hayo na hapendi kuwaona wananchi wa Misri wakikabiliwa na atahari hasi za mapinduzi ya kijeshi.
“Nyoyo zetu zinadunda pamoja na watu wa Misri. Zinadunda pamoja na wale walio katika Medani ya Tahrir na pia wale walio katika Medani ya Rabaa al-Adawiya [medani iliyoko karibu na ikulu ya rais katika mji mkuu wa Misri ambapo wafuasi wa Mursi wamekusanyika]. Ninaamini kuwa wale walio katika Medani ya Tahrir hawaujui ukweli na uhalisia wa mambo. Pindi watakapoujua ukweli wataungana na ndugu zao walio katika (Medani ya) Adawiya,” alisema Erdoğan.
Wiki iliyopita, Erdoğan alitupilia mbali madai ya kwamba Uturuki inachukua msimamo huu dhidi ya mapinduzi ya Misri kwa sababu serikali yake ni mshirika wa Mursi. Alisema kuwa angeendelea kuwa na msimamo huo huo hata kama mapinduzi hayo yangefanywa dhidi ya wale wanaompinga Mursi.
Akielezea maandamano ya bustani ya Gezi, yaliyoanza mwishoni mwa mwezi Mei dhidi ya mpango wa serikali kufanya ujenzi katika Bustani hiyo ya mjini Istanbul na kugeuka kuwa maandamano ya kitaifa ya kuipinga serikali, Erdoğan alisisitiza kuwa matukio ya Misri na Uturuki hayakuwa na tofauti yoyote.
“Chanzo cha matukio katika nchi hizi mbili ni cha aina moja. Nitakitangaza chanzo hicho wakati wa muda muafaka. Nimekihifadhi,” alisema Erdoğan.
Uturuki iliielezea hatua ya jeshi kumuondoa Mursi madarakani kuwa ni “mapinduzi haramu,” katika kutoa msimamo dhidi ya hatua iliyochukuliwa na jeshi la Misri wiki iliyopita. Msimamo huu unaonekana kuwa msimamo wenye nguvu zaidi kutoka nje ya Misri.
Vilevile, Waziri Mkuu wa Uturuki aliendelea kuyakosoa mataifa ya Magharibi kwa kutoiona hatua ya jeshi la Misri kuwa ni “mapinduzi.”
Erdoğan alieleza kuwa tofauti na Uturuki na baadhi ya nchi chache, jumuiya ya kimataifa haikuona mapinduzi hayo kuwa ni “mapinduzi” na wala haikujali mchakato wa kidemkrasia katika taifa hilo la Afrika Kaskazini.
Aidha, Uturuki ilizitaka nchi za Umoja wa Ulaya na taasisi za kimataifa, ikiwa ni pamoja na Umoja wa Mataifa na Umoja wa nchi za Kiarabu, na nchi nyingine pia, kuishinikiza Misri iheshimu na kulinda demokrasia.
Katika hali inayoonesha kuzorota kwa uhusiano wa kidiplomasia baina ya Misri na Uturuki, wiki iliyopita wizara ya mambo ya nje ya Misri ilimuita balozi wa Uturuki nchini humo kwenda kujieleza.

0 comments:
Post a Comment