![]() |
| Wanajeshi wa Misri wakiwa wamesimama mbele ya vifaru vya jeshi nje ya ikulu ya rais mjini Cairo Julai 19, 2013. |
Duru kutoka hospitalini nchini Misri zinasema kuwa waandamanaji watatu wa kike wameuawa katika makabiliano baina ya wapinzani na wafuasi wa rais aliyeondolewa madarakani, Muhammad Mursi katika mji wa Mansura.
Afisa mmoja wa hospitali katika mji huo, Adel Said alisema kuwa watu watatu waliuawa na wengine saba kujeruhiwa kufuatia pande hizo mbili kushambuliana.
Aliongeza kuwa watu wote hao waliouawa jana Ijumaa walikuwa wanawake.
Afisa mwingine wa hospitali katika mji huo, Abdel Wahab Suleiman, alithibitisha idadi hiyo ya vifo na kusema kuwa wanawake hao waliuawa kwa kupigwa risasi.
Aidha, kwa mujibu wa afisa huyo, watu kumi walijeruhiwa na mmoja wao yupo katika hali mbaya.
Maelfu ya waandamanaji walikuwa wakipitia katika mitaa myembamba ya mji huo ndipo "wahuni" walipowashambulia kwa bunduki, visu na mawe, alisema mfuasi mmoja wa Mursi aliyejeruhiwa katika makabiliano.
Jana Ijumaa, maelfu ya wanaharakati wa chama cha Udugu wa Kiislamu na wafuasi wao waliingia barabarani mjini Cairo na katika miji mingine wakitaka Mursi arejeshwe madarakani.
Vilevile, maelfu ya watu waliandamana nchi nzima kuunga mkono mapinduzi ya jeshi dhidi ya Mursi, ambaye alikuwa rais wa kwanza katika nchi hiyo kuchaguliwa kidemokrasia.
Katika hotuba iliyorushwa na vituo vya televisheni usiku wa Julai 3, Mkuu wa Jeshi la Misri, Jenerali Abdel Fattah al-Sisi alitangaza kuwa Mursi, aliyewahi kuwa kiongozi wa chama cha Udugu wa Kiislamu, ameondolewa madarakani na kumtangaza mkuu wa mahakama ya Katiba, Adli Mansour kuwa rais wa mpito. Vilevile, jeshi lilisitisha matumizi ya katiba.
Maafisa wa jeshi walisema kuwa Mursi, ambaye aliingia madarakani Juni 2012, alikuwa ameshikiliwa na jeshi mahali salama.
Mnamo Julai 4, Mansour aliapishwa kuwa rais wa mpito ambapo Julai 5, kiongozi mkuu wa chama cha Udugu wa Kiislamu Muhammad Badie alitangaza kuwa mapinduzi yaliyofanywa dhidi ya Mursi ni batili na kwamba mamilioni ya wafuasi wake wangeendelea kuandamana mpaka atakaporejeshwa madarakani.
Badie aliapa kuendelea mapinduzi yaliyomg'oa rais wa zamani wa nchi hiyo Husni Mubarak mwaka 2011.
Wamisri walianzisha mapinduzi dhidi ya utawala wa Mubaraka Januari 25, 2011, na hatimaye mnamo Februari 11, 2011, utawala huo uliodumu kwa muda wa miaka 30 ukaangushwa.

0 comments:
Post a Comment