![]() |
| Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo |
Mamia ya wananchi wameingia mitaani mjini Goma, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, kumpinga Rais Joseph Kabila kwa kushindwa kuwadhibiti waasi katika eneo hilo.
Maandamano hayo yalifanyika jana Alhamisi katika mji huo katika hali ambayo Umoja wa Mataifa umeelezea wasiwasi wake kuhusu ghasia za hivi karibuni katika eneo hilo.
Mnamo Julai 14, mapambano makali yaliibuka kati ya waasi wa M23 na jeshi la serikali ya Kongo kaskazini mashariki mwa Goma na kuhitimisha wiki kadhaa za utulivu na amani.
Jeshi lilifanikiwa kuwasukuma waasi kilometa kadhaa kutoka mji huo baada ya siku nne za vita na mapambano makali.
Wakati wa maandamano hayo, polisi walitumia gesi ya kutoa machozi dhidi ya waandamanaji waliokuwa na hasira ili kuwatawanya kutoka katikati ya mji wa Goma, ambapo walikuwa wamefunga barabara na kubeba mabango yaliyomtaka Kabila kuondoka madarakani.
Wakati huo huo, ofisi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ilisema katika taarifa yake kuwa mkuu huyo “alisikitishwa mno na ghasia zilizoanzishwa na kundi la M23 kaskazini mwa Goma.”
Taarifa hiyo ilisema kuwa Jeshi la Umoja wa Mataifa la Kulinda amani nchini Kongo (MONUSCO) liko katika hali ya tahadhari kubwa na liko tayari kuingilia kati kupambana na waasi iwapo maisha ya wananchi yatakuwa katika hali ya hatari.
Kikosi Imara chenye askari 3,000 wa Umoja wa Mataifa, ambacho kimepewa jukumu la kupambana na makundi ya waasi ili kurejesha amani nchini humo, kimeanza kufanya doria, lakini hakijaingia katika mapambano.
Waasi wa M23 waliuteka mji wa Goma Novemba 20, 2012 baada ya walinda amani kuondoka katika mji huo wenye wakazi milioni moja. Wapiganaji wa M23 waliondoka katika mji huo Desemba 1,2013 baada ya makubaliano ya kusimamisha mapigano.
Makundi kadhaa yenye silaha, ikiwemo M23, wanaendesha harakati zao za uasi mashariki mwa Kongo na wanapigania kuidhibiti nchi hiyo kubwa yenye maliasili za madini, kama vile dhahabu, urani, coltan, ambayo hutumika katika utengenezaji wa vifaa vingi vya elektroniki, ikiwemo simu za mkononi.

0 comments:
Post a Comment