MISRI: MAHAKAMA YAAMURU MURSI AENDELEE KUSHIKILIWA


Supporters of Egypt’s ousted President Mohamed Morsi hold up his portrait during a demonstration in Cairo on July 24, 2013.



Mahakama nchini Misri imetoa amri kwamba Rais aliyeuzuliwa, Muhammad Mursi, aendelee kuwekwa kizuizini kwa siku 15 zaidi kufuatia mlolongo wa tuhuma mbalimbali zinazomkabili, ikiwemo mauaji ya askari.


Shirika la habari la serikali, MENA, limeripoti kuwa Jaji mpelelezi, Hassan Samir alipata ushahidi wa madai hayo wakati akimhoji Mursi. Hata hivyo, ripoti hiyo haikutaja ni mahali gani au ni lini Mursi alihojiwa.


Mursi anakabiliwa na tuhuma mbalimbali ikiwemo uchomaji, kuharibu rekodi za magereza na "kushirikiana na Hamas (kundi la harakati la Kipalestina) kufanya vitendo vya fujo nchini, kuwashambulia polisi, maafisa na wanajeshi."


Aidha, ripoti hiyo inamtuhumu Mursi kwa "mauaji ya kukusudia na ya kudhamiria dhidi ya  wafungwa, maafisa na askari,"  na kuongezea tuhuma ya "kuwateka nyara maafisa na wanajeshi."


Mursi anadaiwa kuhusika na tuhuma hizo katika nyakati za mwisho za utawala wa Husni Mubarak mapema mwaka 2011.


Mapema mwezi Januari 2011, Mursi na baadhi ya wanachama wa chama cha Udugu wa Kiislamu walitoroka gerezani.
 

Wakati huo huo, msemaji wa chama cha Udugu wa Kiislamu, Gehad El-Haddad, aliziita tuhuma hizo kuwa ni "ujinga" na kusema kuwa hiyo ni ishara ya kurejea madarakani kwa "utawala wa zamani" wa Mubarak.


Wasiwasi umetanda nchini Misri baada ya mkuu wa majeshi, Jenerali Abdul-Fattah al-Sisi, kutangaza Julai 3 kuwa Mursi ameuzuliwa. Pia alisitisha matumizi ya katiba na kulivunja bunge.


Amri hiyo ya mahakama inakuja wakati ambapo Misri inatarajia kushuhudia maandamano makubwa leo Ijumaa yatakayofanywa na wafuasi na wapinzani wa Mursi.


Katika hotuba yake siku ya Alhamisi, Sisi aliitisha maandamano ya nchi nzima ili kulipa jeshi nguvu na mamlaka ya kupambana na kile alichokiita kuwa ni "ghasia na ugaidi," unaoitafuna Misri baada ya kuondolewa kwa Mursi. 


Mpaka sasa Mursi, ameendelea kushikiliwa na jeshi mahali kusikojulikana.


Share on Google Plus

About mahamoud

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment