![]() |
| Waziri Mkuu wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan |
Waziri Mkuu wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amekataa pendekezo la mazungumzo lililotolewa na makamu wa rais wa serikali ya mpito ya Misri, Muhammad ElBaradei, akisema kuwa wadhifa alionao haukutokana na matakwa ya wananchi bali aliteuliwa na utawala wa mapinduzi.
Kwa mujibu wa gazeti la kila siku la Uturuki la Today’s Zamanon, Erdogan alisema kuwa alikuwa wamepokea barua kutoka kwa ElBaradei akiomba kufanya naye mazungumzo kwa njia ya simu kufuatia msimamo wa Waziri Mkuu huyo wa Uturuki kuyakosoa vikali mapinduzi ya kijeshi yaliyotokea nchini Misri.
“Kwa nini nizungumze na wewe? Wewe hukuchaguliwa na wananchi. Wewe ni mtu uliyeteuliwa na utawala wa mapinduzi ya kijeshi," alisema Erdogan akimkusudia ElBaradei wakati wa sherehe moja mjini Ankara.
ElBaradei aliteuliwa kuwa makamu wa rais anayehusika na mahusiano ya kigeni baada ya jeshi kumuondoa madarakani kwa nguvu Rais Mohamed Morsi Julai 3 na kumtangaza mkuu wa Mahakama ya Katiba, Adli Mansour, kuwa rais wa mpito.
Utawala wa mpito unaoungwa mkono na jeshi umechukiwa na hatua ya Erdogan kumuunga mkono Morsi.
Erdogan aliendelea kusema, “Hoja yetu sio Mosri, bali tunamtambua Morsi kama Rais. Bado tunamhesabu Morsi kuwa ndiye rais kwa kuheshimu matakwa ya wananchi wa Misri. Kama ElBaradei angekuwa amechaguliwa na wananchi, ningetumia maneno haya haya ambayo leo ninayatumia kwa Morsi.”
Aidha, Erdogan aliyakosoa mataifa ya Magharibi kwa kutothubutu kulaani kile kilichotokea nchini Misri.
Tangu kuuzuliwa kwa Morsi, Misri imeshuhudia wimbi kubwa la makabiliano makali baina ya wafuasi wa Morsi, wapinzani wake nwa vikosi vya usalama. Kwa uchache watu 100 wameshapoteza maisha katika vurugu na ghasia hizo.
Erdogan alisema kuwa jeshi la Misri lilikusudia "kuhalalisha" mapinduzi kwa kuwaambia watu waandamane, lakini njama hiyo ilishidnwa kwa sababu wapinzani wa mapinduzi hayo nao pia walimiminika mitaani na katika medani ya Rab’a Al-Adawiya mjini Cairo, ambapo wafuasi wa Morsi wamekusanyika kwa wingi.

0 comments:
Post a Comment