30 WAUAWA NA 300 KUJERUHIWA KATIKA GHASIA NCHINI MISRI


Egyptian protesters carry an injured supporter of ousted President Mohamed Morsi after he was shot by security forces outside the headquarters of the Republican Guard in Cairo on July 5, 2013.
Waandamanaji wanamuunga mkono rais aliyeuzuliwa Muhammad Mursi wakimbeba majeruhi baada ya kupigwa risasi na vikosi vya usalama nje ya makao makuu ya Walinzi wa Jamhuri mjini Cairo jana Julai 5, 2013.




Maafisa wa wizara ya Afya ya Misri wamesema kuwa watu thelathini wamepoteza maisha na zaidi ya 300 kujeruhiwa katika maeneo mbalimbali nchini humo kufuatia makabiliano baina ya wapinzani na wafuasi wa rais aliyeondolewa madarakani Muhammad Mursi na vikosi vya usalama.


ALEXANDRIA

Katika mji ulio kandokando mwa bahari ya Mediterranea wa Alexandria, makabiliano makali baina ya waandamanaji yaliripuka baada ya swala ya Ijumaa kufuatia hatua ya jeshi kumpindua Mursi, shirika rasmi la habari la nchi hiyo MENA limeripoti.

Watu kumi na mbili waliuawa na wengine wapatao 200 kujeruhiwa katika vurugu na ghasia zilizotokea mjini Alexandria.

CAIRO

Mjini Cairo, vikosi vya usalama viliwapiga risasi na kuwaua waandamanaji watatu wanamuunga mkono Mursi waliokuwa wakiandamana jana Ijumaa nje ya makao makuu ya Jeshi la Ulinzi wa Jamhuri, hatua iliyoibua makabiliano makali baina ya waandamanaji na vikosi hivyo.


Waandamanaji wanamuunga mkono na wale wanaompinga Mursi walikabiliana pia katika mitaa ya mji wa Cairo na kuwaacha watu kadhaa wakipoteza maisha na wengine kujeruhiwa.


Waandamanaji walisaha moto na kurushiana mawe katika daraja moja jirani na Medani ya Tahrir.

EL ARISH

Katika matukio mengine katika mji wa Sinai ya Kaskazini wa El Arish, polisi watano walipigwa risasi na watu wasiojulikana.

ASSIUT

Katika mji wa kusini wa Assiut, kwa uchache mtu mmoja alifariki kutokana na majeraha ya risasi.

MAAFA

Baadaye jeshi la Misri lilirejesha hali ya utulivu mjini Cairo na katika baadhi ya miji, lakini ghasia zilizotapaa nchi nzima ziliwaacha watu wasiopungua 30 wakiwa wamepoteza maisha na 318 kujeruhiwa, wamesema maafisa usalama.

MSIMAMO WA CHAMA CHA MUSLIM BROTHERHOOD

Mapema hiyo jana, kiongozi mkuu wa chama cha Muslim Brotherhood,  Mohammed Badie alisema kuwa mapinduzi ya kijeshi yaliyofanywa dhidi ya rais wa kwanza kuchaguliwa kidemkrasia nchini humo hayakubaliki kisheria na kwamba mamilioni ya watu wataendelea kuandamana mpaka Mursi atakaporejeshwa mamlakani.

Badie aliyasema hayo wakati akiwahutubiwa maelfu ya wafuasi wa chama hicho waliokuwa wamekusanyika katika msikiti wa Rabia al-Adawiya mjini Cairo.

aliapa “kukamilisha mapinduzi” yaliyoung’oa utawala wa rais wa zamani wa nchi hiyo Husni Mubarak aliyeng’olewa mwaka 2011.

Badie aliendelea kumtaja Mursi kama rais, ambaye aling’olewa madarakani baada ya mamilioni ya watu kuandamana kuupinga utawala wake, akisema kuwa “Mursi ni rais wangu, ni rais wenu na ni rais wa Wamisri wote.”


Aliapa kuwa Mursi atarejea madarakani hivi punde. “Mungu ampe ushindi Mursi na amrejeshe ikulu,” alisema Badie. “Sisi ni askari wake, tutamtetea na kumlinda kwa damu na roho zetu.”

CHANZO CHA HALI YA SASA

Siku ya Jumatano, mkuu wa jeshi la Misri alimvua urais Mursi ambaye aliingia madarakani mwezi Juni 2012, na akaivunja katiba ya nchi katika hatua iliyolenga kuutatua mgogoro wa kisiasa unaoiandama nchi hiyo.

Jenerali Abdel Fattah al-Sisi pia alisema kuwa uchaguzi mpya wa bunge utafanyika hivi karibuni, akamtangaza mkuu wa Mahakama Kuu ya Katiba Adli Mansour kuwa rais wa mpito.

Wamisri walianzisha mapinduzi dhidi ya utawala wa zamani wa Husni Mubarak Januari 25, 2011 na kuuangusha rasmi Februari 11, 2011.


Share on Google Plus

About mahamoud

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment