![]() |
| Adli Mansour, Jaji Mkuu wa Misri na Mkuu wa Mahakama ya Katiba akipigiwa makofi na majaji wenzake baada ya kuapishwa kuwa rais wa mpito wa Misri jana Julai 4, 2013. |
Umoja wa Afrika umeonya kuwa unaweza kusimamisha uanachama wa Misri kufuatia kwenda kinyume na utawala wa katiba kulikofanywa na jeshi la nchi hiyo na kumuondoa madarakani Rais Muhammad Mursi.
Jana Alhamisi Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika lilitangaza kuwa maafisa watakutana leo Ijumaa kuzungumzia hali ya mambo nchini Misri na kuchukua hatua inayoweza kusitisha uanachama wa nchi hiyo.
Rais wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, bibi Nkosazana Dlamini-Zuma alisema kuwa hatua ya jeshi kumuondoa Mursi “niuvunjaji wa mamlaka ya kikatiba ya Misri na ni kinyume na misingi ya Umoja wa Afrika inayopinga mabadiliko ya kiserikali yasiyokuwa ya kikatiba.”
Dlamini-Zuma aliwataka Wamisri kuheshimu sehria na kufanya mazungumzo ili kukomesha mzozo wa kisiasa unaowakabili.
Taarifa hiyo ya Umoja wa Afrika limeungwa mkono na viongozi wengine wa Kiafrika, akiwemo Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta aliyesema kuwa, “Kinachotokea sasa Misri ni jambo lenye kuogofya sana sio tu barani Afrika, bali linatakiwa kumpa wasiwasi kila muumini wa mfumo wa kidemokrasia.”
Mnamo Julai 3, Jenerali Abdel Fattah al-Sisi, mkuu wa majeshi ya Misri, alitangaza kumuondoa madarakani Rais Mursi.
Jaji mkuu wa Mahakama Kuu ya Katiba, Adli Mansour, aliapishwa jana kuwa rais wa mpito.
Itakumbukwa kuwa mwezi Machi Umoja wa Afrika ulisitisha uanachama wa nchi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati baada ya wapiganaji watiifu kwa kiongozi wa kundi la Seleka Michel Djotodia kuiondosha serikali madarakani.

0 comments:
Post a Comment