
Mkuu wa Jeshi la Libya amejiuzulu kutokana na mapigano yaliyotokea Benghazi, mashariki mwa nchi hiyo.
Shirika la Habari la FARS limeripoti kuwa, Meja Jenerali Youssef al-Mangoush leo amejiuzulu kufuatia kutokea mapigano jana Jumamosi katika mji wa Benghazi na kupelekea makumi ya watu kuuawa na kujeruhiwa.
Mapigano hayo yalitokea kati ya wakazi wa eneo hilo na wanamgambo ambao walishiriki katika mapinduzi yaliyomng'oa madarakani Kanali Muammar Gaddafi wa nchi hiyo.
Wakati huo huo Bunge la Libya limewataka wananchi wa Libya wajiepushe na fitna. Mwito huo umetolewa baada ya kutokea mapigano katika aneo la al Kufiyyah, huko Benghazi, mashariki mwa Libya na kupelekea watu 28 kuuawa.
Gazeti la al Qudsul Arabi limenukuu taarifa ya Bunge la Libya ikisema kuwa, bunge hilo linafuatilia kwa karibu matukio hayo na linawasiliana mara kwa mara na serikali ili kutafuta njia za kutatua matatizo yaliyopo.
Vile vile bunge la Libya limesema katika taarifa yake hiyo kwamba, makundi na mirengo yote ya kisiasa na taasisi za kijamii yanapaswa kujiweka mbali na fitna na badala yake zikae pamoja kwa ajili ya kutafuta ufumbuzi wa matatizo yao.
Aidha limesema, matatizo hayawezi kutatuka bila ya watu kutekeleza vizuri majukumu yao na kwamba kundi lolote lile halipaswi kufanya njama za kulitoa uwanjani kundi jingine, bali makundi yote yashirikiane kutatua matatizo hayo.
Wakati huo huo Waziri Mkuu wa Libya, Ali Zaidan, amegusia sababu za kutokea mapigano kati ya wanamgambo na wakati wa eneo la al Kufiyyah huko Benghazi na kusema kuwa mapigano hayo yameisha.
Taarifa nyingine zinasema kuwa, makumi ya watu wameuawa na kujeruhiwa katika mapigano hayo.
0 comments:
Post a Comment